In Summary

Katika swali la msingi Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) Selemani Bungara amehoji Serikali imetenga kiasi gani cha fedha 

Dodoma. Serikali imesema tatizo la wanafunzi wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam kutopewa vyeti vyao baada ya kuhitimu mafunzo yao limeshafikishwa na wanashughulikia.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema hayo leo Juni 14 bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Temeke (CUF) Abdallah Mtolea.

Mtolea amesema kutokana na kutopewa kwa vyeti kwa wahitimu wa chuo hicho wanashindwa kuajirika na kuhoji ni lini Serikali italishughulikia tatizo hilo.

Akijibu Ole Nasha amesema tatizo hilo limeshafikishwa wizarani kwake na wanalishughulikia na kwamba wakikamilisha watajulishwa.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Mpwapwa (CCM) George Lubeleje amesema Serikali imekuwa ikitoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha nne lakini kidato cha tano na Sita wanalipia.

"Hawa ni watoto wa mtu mmoja, je ni lini Serikali itatoa elimu bure kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita?" Amehoji.

Akijibu swali hilo, Nasha amesema Serikali itatoa elimu bure kwa wanafunzi wa kidato cha tano hadi sita na hadi vyuo vikuu uwezo utakavyoongezeka.

"Kwasasa kutokana na hali ya fedha tunaimarisha miundombinu. Tunatoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ya Sh427 bilioni kila mwaka,"amesema.

Katika swali la msingi Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) Selemani Bungara amehoji Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pamoja samani nyingine chuoni hapo.

Akijibu swali hilo, Nasha amesema Serikali imetoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu.

“Taratibu za ukarabati zitaanza baada ya kukamilika kwa zoezi hili. Pia wizara anafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika vyuo vya maendeleo ya wananchi zoezi linatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu," amesema.