In Summary
  • Shahidi huyo wa 26 ambaye ni mkemia kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kaijunga Brassy alitoa ushahidi wake jana, baada ya Jaji Salma Maghimbi kuridhia ombi hilo.

Moshi. Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto Msuya, umeongeza shahidi wa ziada katika kesi hiyo ambaye hakuwamo katika orodha ya mashahidi 50 wa Jamhuri.

Shahidi huyo wa 26 ambaye ni mkemia kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kaijunga Brassy alitoa ushahidi wake jana, baada ya Jaji Salma Maghimbi kuridhia ombi hilo.

Kabla ya kuanza kwa shauri hilo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, uliwasilisha mahakamani ilani ya kumuita shahidi huyo wa ziada.

Wakili Chavula ambaye anasaidiana na wakili Kassim Nassir, alisema ushahidi wa shahidi huyo katika notisi hiyo na kwa mujibu wa notisi hiyo ulihusu vipimo vya vinasaba (DNA).

Shahidi huyo ndiye aliyechukua sampuli za mate na damu kutoka kwa mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir na sampuli kutoka kwenye jaketi.

Ombi la kumuongeza shahidi huyo wa ziada halikupingwa na jopo la mawakili wa utetezi linalowajumuisha Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na John Lundu.

Hata hivyo, wakati shahidi huyo alipotaka kutoa jaketi alilolitumia kuchukua sampuli ili zikaoanishwe na sampuli za damu na mate, kama kielelezo, kuliibuka ubishani mkali wa kisheria.

Akitoa ushahidi wake jana kwa kuongozwa na wakili Nassir, shahidi huyo alidai Septemba 19, 2013 akiwa katika ofisi za mkemia mkuu Kanda ya Kaskazini, walifika polisi kutoka Moshi.

Alieleza kuwa polisi hao wakiongozwa na mkaguzi msaidizi wa polisi, Damian Chilumba, walifika wakiwa na kielelezo ambacho ni jaketi la rangi ya kaki na watuhumiwa hao wawili.

“Aliniambia (Chilumba) kuwa ana kielelezo ambacho ni jaketi la rangi ya kaki na watuhumiwa ambao walitakiwa kuchukuliwa sampuli za DNA ili kuzioanisha na kielelezo hicho,” alidai.

Jaketi hilo ndilo ambalo shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Raphael Karoli alidai mahakamani alipotoa ushahidi wake Oktoba 6, 2015, kuwa liliachwa na watu wawili wenye silaha.

Shahidi huyo wa 26 alidai baada ya kupokea kielelezo hicho alilifungua na kuangalia ni maeneo gani ambayo anaweza kupata seli kwa ajili ya kupima DNA.

“Kulikuwa na maeneo matano ambayo tungeweza kupata seli ambayo ni mifuko ya nje, juu ya mfuko, mfuko wa juu, mikono ya jaketi na upinde (collar) wa hilo jaketi,” alidai shahidi huyo na kuongeza:

“Tulikuwa tunatafuta maeneo yenye jasho ili kupata seli ambazo zingetusaidia kupima DNA.  Kila kipande nilichokata kwenye koti nilikifunga kwenye bahasha yake na kuiwekea label (alama)”.

Shahidi huyo alidai baada ya kukamilisha uchukuaji sampuli hizo, waliletwa washtakiwa hao wawili ambao alichukua sampuli za damu na mate kwa kila mmoja na kuzifunga tofauti tofauti.

“Sampuli zote nilizihifadhi vizuri na Oktoba 2, 2013 nilizisafirisha kwenda ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu Dar es Salaam na kumkabidhi Gloria Omari (shahidi wa 25 wa mashtaka),” alidai.

Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee fomu ya makabidhiano ya jaketi hilo kutoka kwa Inspekta Chilumba kwenda kwake, ombi ambalo halikupingwa na jopo la mawakili wanaowatetea washtakiwa.

Hata hivyo, wakati shahidi huyo alipoiomba mahakama ipokee jaketi hilo kama kielelezo, uliibuka ubishani wa kisheria baada ya mawakili wa utetezi kupinga vikali kupokelewa kwake.

Akiwasilisha hoja za kupinga kupokelewa kwa jaketi hilo, wakili Magafu alidai hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaoonyesha Inspekta Chilumba alilitoa wapi koti hilo hadi kumkabidhi shahidi.

“Ametuonyesha fomu (kielelezo namba 18) kuwa alilipata hilo jacket kwa Inspekta Chilumba, lakini hakuna ushahidi wa chain of custody (muunganiko wa makabidhiano) ya kielelezo hiki,” alidai Magafu na kuongeza:

“Hatujaletewa exhibit register (kitabu cha kutunza vielelezo) kutoka upelelezi Moshi kinachoonyesha jaketi hili ni miongoni mwa vielelezo vilivyokusanywa kutoka eneo la tukio.

“Hoja nyingine ni kuwa shahidi wa tatu (Karoli) alitoa ushahidi wake hapa Oktoba 6, 2015 na alionyesha jaketi likiwa ni zima na halikuwa limekatwa vipande vipande kama hili.

“Shahidi leo (jana) anatwambia aliletewa hili koti Septemba 19, 2013 lakini Oktoba 6, 2015 Karoli alionyeshwa likiwa zima hivyo haya ni makoti mawili tofauti. Hili kalitoa wapi?”

Wakili Magafu aliieleza mahakama kuwa wakati shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka, Inspekta Samwel Maimu alipotoa ushahidi wake, alidai ndiye aliyekusanya vielelezo vyote eneo la tukio.

“Ushahidi wa shahidi wa tisa alisema yeye ndiye alikusanya vielelezo vyote eneo la tukio, hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha jaketi lilimfikiaje Chilumba ili alipeleke kwa shahidi wa 26,” alidai.

Kutokana na hoja hizo, mawakili hao waliiomba Mahakama isipokee jaketi hilo kama kielelezo, hoja ambazo zilipingwa na mawakili wa Serikali.

Akijibu hoja, Chavula alidai ni mapema mno kuzungumzia namna koti hilo lilivyomfikia Inspekta Chilumba.

“Ni mapema mno kuzungumzia hili kwa sababu Chilumba hajatoa bado ushahidi wake unaoonyesha namna koti hilo lilivyomfikia. Chilumba hajaja kutoa ushahidi kwenye hii kesi,” alidai.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Maghimbi aliiahirisha kesi hiyo hadi leo saa 3:00 asubuhi ambapo atatoa uamuzi mdogo kama jaketi hilo lipokelewe kama kielelezo cha kesi ama la.