In Summary

Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika alisema ajira kwa watumishi wa umma hutolewa kutegemeana na bajeti ya Serikali.

Dodoma. Serikali imesema mwaka 2018/19 itatoa ajira mpya 49,356 ambazo ni mbali ya zile 52,000 ilizoahidi mwaka 2017/18 ambazo mpaka sasa imeajiri watu zaidi ya 18,000.

Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika alisema ajira kwa watumishi wa umma hutolewa kutegemeana na bajeti ya Serikali.

Alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ambayo iliwasilishwa bungeni Jumatano iliyopita na kujadiliwa na wabunge kwa siku nne.

Alisema bajeti inaporuhusu Serikali imekuwa ikitoa ajira na kwa mwaka ujao wa fedha unaoanzia Julai, watu 49,356 wataajiriwa wakiwamo walimu 16,000 wa shule za msingi na sekondari, kada ya afya nafasi 15,000 na nafasi zilizobaki zitakuwa ni kwa ajili ya kada nyingine ikiwemo kilimo, uvuvi, mifugo, vyombo vya ulinzi, magereza, uhamiaji, watendaji na wahadhiri. Mkuchika alisema hadi kufikia mwezi Machi, Serikali imeajiri watumishi zaidi ya 18,000 kuziba maeneo yenye upungufu mkubwa.

Aliongeza kuwa, katika mwaka huo walipanga kuajiri watumishi 52,000 ambapo wengi wao ni wa idara za elimu, afya na Serikali za mitaa.

“Hawa tunaowaajiri (wabunge) mmeshawapitisha katika bajeti iliyopita. Hawa ni tofauti na 49,356 tutakaowaajiri mwaka wa fedha 2018/19,” alisema.

Alibainisha kuwa ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa kuajiri kulisimama wakati wa uhakiki wa vyeti ambao umeshakamilika.

Mkuchika alisema tayari Serikali imeajiri watumishi mbadala wa walioondolewa kwa vyeti feki na utaratibu wa kuziba nafasi zilizo wazi unakaribia kukamilika.

Kuhusu watumishi kupandishwa vyeo alisema, “Kama ilivyo kwa suala la ajira, upandishaji wa vyeo hutegemea sifa za muundo wa utendaji mzuri, bajeti ya mishahara.”

Mkuchika alisema Serikali katika mwaka wa fedha ujao imetenga nafasi 162,221 za watumishi watakaopandishwa vyeo kulingana na sifa.

Alibainisha kuwa katika nafasi hizo, 2,044 zimetengwa kwa ajili ya kuziba mapengo mbalimbali katika ngazi ya madaraka.

Kuhusu wabunge kulalamikia vitendo vya utekaji na kupigwa, alisema Serikali haiungi mkono matukio hayo. “Jeshi lenye dhamana na usalama wa raia ni la polisi na si Idara ya Usalama wa Taifa. Natoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema Mkuchika.

Pia aligusia hoja ya wabunge kuhusu kukiukwa kwa Katiba ya nchi ikiwemo kuzuia mikutano ya hadhara akisema, “Taasisi yoyote inayoona inanyimwa haki yake kikatiba ina nafasi ya kupeleka malalamiko katika vyombo vinavyotoa haki ambavyo ni mahakama.”

Vilevile Mkuchika alijibu hoja ya wabunge kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande watu wa kada mbalimbali na kubainisha kuwa Sheria ya Utawala ya Mwaka 1997 imewapa viongozi hao mamlaka ya kuwaweka mahabusu watu kwa saa 24, ikiwa wanabainika kutenda makosa yoyote yenye kuhatarisha amani na utulivu kwa jamii.

Serikali yaongeza fedha elimu bure

Katika hatua nyingine, Serikali ilitangaza kuongeza Sh3.6 bilioni katika fedha zinazotengwa kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo.

Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema uamuzi huo unatokana na baadhi ya wabunge kulalamika kuwa fedha hazitoshi.

“Hata sisi wizara tulikwama,” alisema Jafo.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja za wabunge zilizoibuliwa wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi yake na kwamba, kuanzia Desemba 2015, Serikali ilikuwa ikitoa bajeti ya elimu bila malipo ya Sh23 bilioni kila mwezi.

“Tulimuomba Rais akasema tusubiri bajeti hii na bahati nzuri sasa tumepata addition (nyongeza) ya fedha karibuni Sh3.6 bilioni ambayo inaongezeka katika bajeti,”alisema Jafo.