In Summary

Sam atazikwa kesho saa 9.00 nyumbani kwao Kiwangwa Bagamoyo

Muimbaji Sam wa Ukweli amefariki leo Juni 6, 2018, baada ya kuzidiwa ghafla akiwa studio ya Asound Record iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na MCL Digital, aliyekuwa meneja wake, Amri Aliamini amesema, Sam alizidiwa jana saa 2.05  usiku akiwa anarekodi ,akapelekwa Hopitali ya Palestina lakini inaelezwa alifariki akiwa njiani.

Aliamini anasema kabla ya hapo alikuwa anasumbuliwa mara kwa mara  na  Marelia na  homa ya manjano mwezi mmoja na nusu akiwa Singida kwenye shoo.

"Mimi nachojua chanzo cha kufariki Sam ni kuumwa malaria na homa ya manjano, amefariki jana usiku akiwa njia anapelekwa hospitali, baada ya kuzidiwa akiwa studio ya Asound iliyopo Mabibo, tulipofika Hospitali ya Palestina akahifadhiwa kwa muda na baadae tukaambiwa tumpeleke Mwananyamala maana pale hawahifadhi," anasema.

Anaongeza kuwa Sam atazikwa kesho saa 9.00 nyumbani kwao Kiwangwa Bagamoyo, lakini leo watafanya kikao saa 6.00 mchana kwa mjomba wake anayeitwa Saidi Yanga anayeishi  Tandale.