In Summary
  • Hali hiyo iliibuka bungeni asubuhi baada ya wabunge kuomba mwongozo na kuhoji kama kinachofanywa na mawaziri hao ni sahihi au la, na kutaka kiti cha Spika kutoa ufafanuzi.

Dodoma. Kitendo cha mawaziri kuendelea kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jana kimeligawa Bunge na Serikali baada utaratibu huo kuhojiwa na wabunge huku Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akisema wanachokijibu ni maoni yao binafsi.

Hali hiyo iliibuka bungeni asubuhi baada ya wabunge kuomba mwongozo na kuhoji kama kinachofanywa na mawaziri hao ni sahihi au la, na kutaka kiti cha Spika kutoa ufafanuzi.

Dk Tulia alisema kuwa, licha ya kila mtu kuwa huru kujadili ripoti ya CAG, mawaziri wanapaswa kutoa majibu katika kamati za Bunge.

Wakati wabunge wakihoji ukaguzi huo ulioishia Juni 30, 2017, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina baada ya kipindi cha maswali na majibu walizungumza na waandishi wa habari na kujibu ripoti hiyo ya CAG katika maeneo yanayohusu wizara zao.

Muda mfupi baada ya mawaziri hao kutoa ufafanuzi, Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Vedasto Mwiru na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka walizungumza na wanahabari na kupinga kitendo kinachofanywa na mawaziri hao.

Kaboyoka alisema kinachofanywa na mawaziri si sahihi kwa sababu wanaopaswa kujibu taarifa ya CAG ni makatibu wakuu wa wizara, wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa mashirika na taasisi za Serikali.

Majibu ya Mpina na Dk Tizeba yanafanya idadi ya mawaziri waliojibu ripoti ya ukaguzi ya CAG tangu alipoiwasilisha bungeni Aprili 11, kufikia sita.

Mawaziri wengine ni wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe; wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage; wa Fedha, Dk Philip Mpango na wa Tamisemi, Selemani Jafo.

Wabunge wahoji

Katika mwongozo aliouomba kwa kiti cha Spika jana, Stanslaus Mabula (Nyamagana-CCM) alisema, “Ripoti ya CAG imezua mjadala bungeni na nje ya Bunge, hasa mawaziri wanapoeleza masuala mbalimbali. Wananchi wanachanganyikiwa, ninataka mwongozo wako ni sawa ama si sawa.”

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga aliungana na Mabula na kusema, “mawaziri wanajibu wapendavyo…sasa nataka kujua mwongozo wako, nini kauli ya kiti chako ina maana baada ya wao kutoa kauli hii, hili suala ndio limekwisha. Kama ni hivyo na mimi nataka nijipange na wana Ulanga, ili kujua na sisi tunakujaje kutokana na ripoti hiyo ya CAG.”

Akijibu miongozo ya wabunge hao, Dk Tulia alisema kujadili taarifa ya CAG si dhambi, lakini mawaziri wanapaswa kutoa majibu katika kamati za Bunge na kwamba, wanachofanya sasa ni kutoa maoni yao binafsi. Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma, mawaziri wanapaswa kutoa majibu katika vikao vya kamati za Bunge.

“Sheria kama ambavyo haimkatazi CAG kuzungumza na vyombo vya habari, kwa namna hiyohiyo haimkatazi mtu yeyote kuzungumzia taarifa ya CAG, haijasema CAG azungumze na vyombo vya habari na pia haijamkataza mtu yeyote kuzungumzia taarifa hii,” alisema.

“ Sheria hizi mkizipitia waheshimiwa wabunge mtaona, majibu huwa hayatolewi kwa mdomo. Mawaziri wanatoa mawazo yao.

“Kwa hiyo waziri anavyotoa maelezo si kwamba amejibu hoja za CAG, hoja za CAG zinajibiwa kwenye kamati kwa mujibu wa sheria. Anayejibu kwenye kamati ni ofisa masuhuli husika. Msitake kuliweka hili jambo kuonyesha hakuna utawala wa sheria nchini. Sheria zipo na mzisome vizuri kuliko kutoa maelezo ya kuchanganya umma.”

Mawaziri wajibu

Katika maelezo yake kwa wanahabari, Dk Tizeba alieleza mambo matano yaliyotajwa katika taarifa ya CAG ambayo ni uwepo wa viuatilifu visivyosajiliwa sokoni, uwepo wa wakaguzi mipakani wasiokuwa na ujuzi wa kutosha kusimamia viuatilifu, upimaji usiotosheleza wa afya na mazingira kuhusiana na matumizi ya viuatilifu na taarifa kwa umma kuhusu viuatilifu vilivyosajiliwa na vilivyoondolewa kwenye orodha ya usajili.

“Taarifa ya CAG imeainisha upungufu katika usimamizi wa viuatilifu kwa manufaa ya wakulima na nchi. Ushauri uliotolewa utatuwezesha kuchukua hatua zilizopendekezwa katika kuleta tija katika shughuli za kilimo,” alisema Dk Tizeba.

Kwa upande wake, Mpina alizungumzia jinsi taarifa ya CAG ilivyobainisha upungufu katika usimamizi wa hifadhi za bahari na maeneo tengefu ikiwemo hifadhi za bahari maeneo ya Tanga na Mtwara kutozingatia kanuni za utoaji wa vibali vya matumizi ya rasilimali.

“Jambo hili linatokana na udhaifu wa menejimenti ya bodi ya wadhamini ya kitengo cha bahari na maeneo tengefu. Kwa mamlaka niliyonayo namsimamisha kazi Meneja Kitengo cha Bahari na Maeneo Tengefu, Dk Milali Machumu kwa kushindwa kusimamia ipasavyo kitengo hicho. Pia navunja bodi ya wadhamini ya kitengo hicho,” alisema.

Awali, kiongozi wa msafara wa mawaziri hao, Dk Mwakyembe alisema sheria ya ukaguzi hamzuii waziri kueleza kilichoainishwa.