In Summary

Kati ya kolabo zinazovuta hisia nyingi za mashabiki na kuweka kumbukumbu kwenye vichwa vyao


Kati ya kolabo zinazovuta hisia nyingi za mashabiki na kuweka kumbukumbu kwenye vichwa vyao, basi ni zile za wanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond Plutnumz na Rayvanny.

Ishu iko hivi…wanamuziki hawa wameshatoa kolabo mbili matata zenye kuacha maswali na kumbukumbu kwenye vichwa vya mashabiki na kujiuliza kwa nini huwa inatokea hivi.

Maswali hayo na kumbukumbu yanatokana na kolabo ya wimbo wa ‘Salome’ na ‘Iyena’ ambazo Diamond amemshirikisha Rayvanny.

Katika kolabo ya kwanza ya wimbo wa ‘Salome’ iliacha kumbukumbu pale mrembo Hamisa Mobetto alipowekwa kama Video Queen katika wimbo huo, huku kuwepo kwa fununu za wawili hao kutoka kimapenzi.

Kwa nyakati tofauti Diamond alikanusha kutoka na Hamisa Mobetto hata baada ya mwanamke huyo kuwa na ujauzito.

Katika mahojiano mbalimbali likanusha kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi mpaka baada picha na video kuanza kuonekana katika mitandao ya kijamii huku ikielezwa kuwa Hamisa ndiye aliyevujisha.

Baadaye Diamond alikubali yaishe kwa kukiri kuwa mtoto wa mwanamke huyo ni wake hata hivyo, akisema kilichobaki ni uhusiano katika malezi na si vinginevyo.

Wimbo wa Iyena

Kwa upande wa wimbo huu wa ‘Iyena’,mambo ni yaleyale, Zari na Diamond waliachana Februari 14, mwaka huu, siku ya wapendanao. Zari ndiye aliyetamka kuwa anamuacha Diamond kutokana na kumdhalilisha kwa kuwa karibu na wanawake alioachana nao ikiwa ni siku chache tangu alipoonekana akiwa na Wema Sepetu.

Baada ya sakata hilo, Diamond ameachia wimbo huo ambao ndani yake Zari ameupamba kama video queen na kuamsha upya mashabiki wao wakitaka warudiane.

Wimbo huo ndio umeleta maswali kwenye vichwa vya mashabiki kwamba kila akimshirikisha Rayvanny huwa inatokea tukio linalotikisa uhusiano wa mwanamuziki huyo.

Kutoka kwa wimbo huo wa Iyena,umekuwa kama wimbo wa Salome ulivyowarudisha Diamond na Hamisa ndio imekuwa kwa Zari.