In Summary

Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza amesema wamealikwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi kwa ajili ya kula pamoja chakula cha mchana

Dodoma. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli leo Jumatatu Aprili 15, 2019 amekutana na wabunge wa chama hicho jijini Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza amesema walialikwa na kiongozi huyo mkuu wa nchi  nyumbani kwake kwa ajili ya kula naye chakula cha mchana.

“Amewaalika wabunge wa CCM leo mchana kula chakula, tumesalimiana na kupeana hongera ya kazi,” amesema Rweikiza.

Wakati huo huo, kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho tawala (NEC) imekutana leo jijini hapa chini ya uongozi wa Rais Magufuli na kumteua John Pallangyo kuwa mgombea ubunge wa Arumeru Mashariki.

Uchaguzi katika jimbo hilo unafanyika baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kuwa jimbo hilo lipo wazi kutokana na Joshua Nassari (Chadema) kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge kwa kutohudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo.

Taarifa iliyotolewa na katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole imesema pia, kikao hicho kimefanya uteuzi wa wajumbe wanaogombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kundi la Bara ambao ni Sara Sompo, Japhary Mghamba na Ngusa Juda.