In Summary

Polisi katika mji wa Barcelona wamesema wanawasaka watu wasiofahamika waliovunja na kumwibia mlinzi wa timu ya Barcelona, Jordi Alba, vitu mbali mbali ambavyo bado havijajulikana idadi yake wala thamani jana usiku wakati mchezaji huyo akiwa Italia kuitumikia timu yake katika Ligi ya Mabingwa UIaya.


Barcelona, Hispania. Polisi katika mji wa Barcelona, wapo kwenye hekaheka wakiwasaka wezi waliovunja na kuiba vitu mbali mbali kwenye nyumba ya mlinzi wa timu ya Barcelona, Jordi Alba.

Wezi hao walifanya kitendo hicho jana usiku wakitumia mwanya wa mchezaji huyo kutokuwepo nyumbani.

Alba pamoja na wachezaji wengine wa timu hiyo walikuwa mjini Milan Italia kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan, ulioisha kwa sare ya bao 1-1.

Kwa mujibu wa gazeti la La Vanguardia, wezi hao walivunja dirisha lililopo bustanini na kuingia ndani ambako walipita chumba moja baada ya kingine na kuiba vitu mbali mbali ambavyo thamani yake bado haijajulikana.

Mke wa mchezo huyo na watoto walikuwepo nyumbani wakati wizi huo ukitokea lakini hawakudhuriwa huku walinzi wa nyumba hiyo wakiwa hawajui chochote kilichotokea usiku huo.

Mlinzi aliyekuwa nyumbani hapo anadai kutosikia wala kujua chochote hadi alipoarifiwa asubuhi na polisi kuwa katika nyumba aliyolinda ulifanyika wizi.