In Summary

Wasema hata alipochunguzwa hakuwa na majeraha na alikuwa na afya njema

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na polisi mkoani Iringa limebaini na kujiridhisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo hakutekwa, bali ‘alijiteka’ mwenyewe

Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema polisi watachukua hatua za kisheria  kwa kuwa mwanafunzi huyo amewadanganya watu kuwa ametekwa na kusababisha taharuki kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Mambosasa amesema polisi wamefanya uchunguzi na kubaini mwanafunzi huyo hakutekwa bali ‘alijiteka’ mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kusababisha kuzua tafrani kwa jamii.

Amesema Machi 6, 2018 saa sita usiku zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Nondo ametekwa na watu wasiojulikana.

Amebainisha kuwa polisi wa kdana hiyo walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo ikiwa pamoja na kufunguliwa jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.

Mambosasa amesema Machi 7, 2018 walipewa taarifa na polisi mkoani Iringa kuwa mwanafunzi huyo ameonekana Wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake.

“Mwanafunzi huyu alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa katika kituo chochote cha polisi hivyo tunaendelea kumshilikia hivyo taratibu ili tumpeleke mahakamani,”amesema Mambosasa.

Amesema upelelezi umebaini mwanafunzi huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye mawasiliano mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa.

Mambosasa amesema kuwa pia alivyopimwa alionekana mwenye afya njema, hakupewa dawa yoyote ya kumlevya na hakuwa na majeraha.