In Summary

Amesema ushindi huo unatokana na mikutano ya kampeni ya chama hicho tawala kuwa na idadi kubwa ya wananchi kuliko ile ya vyama vya upinzani

 

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama chake kitashinda uchaguzi mdogo katika majimbo ya Ukonga na Monduli unaotarajia kufanyika Septemba 16, 2018.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 14, 2018 Polepole amesema CCM imefanya kampeni za kistaarabu na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuwasikiliza.

"Tathmini ya awali inaonyesha kwamba mikutano yetu ya hadhara ilikuwa mikubwa mara tatu kuliko ile waliyofanya wenzetu," amesema.

Polepole amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kukichagua chama tawala li kiwaletee maendeleo kwenye maeneo yao.

"Wachague wagombea wa CCM ili wakawe kiungo na Serikali katika kutatua kero zao. Ukichagua mgombea wa CCM, atashirikiana na viongozi wa Serikali kuleta maendeleo," amesema.

Polepole amesema chama chake kinatoa elimu juu ya sheria za uchaguzi. Pia, amesema wanatoa elimu juu ya kanuni za uchaguzi za CCM.

Amesema katika awamu hii, CCM imejipanga kufanya siasa safi za kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo. Amesema chama chake kimejipanga kutatua kero mbalimbali.