In Summary

Sasa iko hivi, England ambayo imeingia nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 1990

CROATIA imetisha. Imeingia fainali kibabe baada ya kuibandua England kwa mabao 2-1, mchezo ulioamuliwa baada ya dakika 109.

Mchezo huo uliochezwa kwa dakika 120, lakini straika wa Juventus, Mario Mandzukic alitumia dakika 109 kumaliza kazi kwa kupachika bao la pili lililoimaliza England. Awali Kieran Trippier alifungia England bao la kuongoza dakika ya tano tu kabla ya Ivan Perisic kusawazisha dakika ya 68.

Sasa iko hivi, England ambayo imeingia nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 1990, haitarudi kwao England, watakwenda kwenye Uwanja wa Saint Petersburg Jumamosi kucheza na Ubelgiji ambayo nayo iliifungwa bao 1-0 na Ufaransa katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa Jumanne usiku.

England na Ubelgiji zilikutana hatua ya makundi, kusaka mshindi wa kwanza na wapili na England ililala kwa bao 1-0 na safari hii wanasaka mshindi wa tatu na nne.

Croatia iliyoingia fainali mara ya mwisho 1998 ikiwa na mastaa wake kama Ivan Rakitic, Mateo Kovacic, Milan Badelj itakuwa na kibarua pevu dhidi ya kikosi cha wakali wa Ufaransa Jumapili kikiwa na watu kama N’Golo Kante, Olivier Giroud, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe lakini siku hiyo macho yote yatakuwa kwa mastaa wa timu hizo, Ufaransa ikiwa na kiungo wake matata, Paul Pogba huku Croatia ikiwa na Luka Modric.

Fifa tayari imetangaza mzigo wa maana kwa bingwa kwani mwaka huu umeongezeka kutoka Dola 358 milioni zilichukuliwa na Ujerumani 2014 katika fainali za Brazil, lakini bingwa wa mwaka huu, atalamba Dola400 milioni (Sh852 bilioni fedha za Tanzania).