In Summary

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemburuza kortini  ofisa manunuzi wa Wakala wa Barabara (Tarura) Manispaa ya Moshi, Samwel Mseselo kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh7.7milioni


Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemburuza kortini  ofisa manunuzi wa Wakala wa Barabara (Tarura) Manispaa ya Moshi, Samwel Mseselo kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh7.7 milioni za uchaguzi wa mkuu wa 2015.

Taarifa iliyotolewa jana Oktoba 11, 2018 na mkuu wa Takukuru Mkoa Kilimanjaro, Holle Makungu, imesema ofisa huyo ameshitakiwa kwa makosa sita ya uhujumu uchumi aliyoyafanya mwaka 2015 akiwa Afisa Manunuzi Halmashauri ya wilaya ya Siha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ofisa huyo ameunganishwa na wafanyabiashara wawili, Fatuma Kanunga na Fredrick Kitali ambao inadaiwa nyaraka za kampuni zao zilitumika kufanya udanganyifu huo.

Watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Siha Mfawidhi, Jasmin Athman na kusomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka wa Takukuru, Rehema Mteta.

Katika mashitaka yanayomkabili ofisa manunuzi wa Tarura, upande wa mashitaka umedai mwaka 2015, alifanya udanganyifu wa nyaraka kuonyesha Halmashauri ilipokea huduma ya Sh1.6 milioni kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.

Pia,  mtuhumiwa huyo ameunganishwa na Fatuma katika shitaka lingine kwamba alitumia nyaraka za udanganyifu kuonyesha Sh3.9 milioni zililipwa kwa Embassy Tea Room kwa ajili ya kukodi mahema 30.

 

Katika shitaka la nne, Mseselo ameunganishwa na Fatuma, wakituhumiwa kufanya ubadhirifu wa Sh1.7 milioni wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika mwaka 2015.

 

Katika shitaka la tano na sita, ofisa manunuzi huyo wa Tarura ameunganishwa na mtuhumiwa Kitali anayemiliki duka la kuuza vipuri la Kitali Auto Spares wakituhumiwa kufanya ubadhirifu wa Sh521,000.

 

Watuhumiwa wote wamekanusha mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana hadi Novemba 12, 2018 wakati kesi yao itakaposikilizwa kwa hatua za awali kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

 

Wakati huo huo mahakama ya wilaya ya Siha, imemhukumu kifungo cha miaka saba au kulipa faini ya Sh2 milioni, mwenyekiti wa kijiji cha Miti Mirefu wilayani humo,Matei Komu kwa tuhuma za ubadhirifu wa sh7 milioni.

 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa wilaya ya Siha Mfawidhi,  Jasmin Athman baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kujipatia  fedha hizo kwa njia udanganyifu, mashitaka yaliyokuwa yamefunguliwa na Takukuru.