In Summary

Sura pekee zenye huzuni katika michuano ya Kombe la Dunia ni zile ambazo timu zao zimefungwa.

WIKI moja ya maisha yako. Nenda popote pale inapofanyika michuano ya Kombe la Dunia hata kama hauna tiketi. Hautasahau. Inafurahisha. Haikinaishi. Wote waliopita Russia katika nyakati hizi siku moja watakwambia ambavyo hawatasahau.

Nilikwenda Kombe la Dunia Afrika Kusini. Nilikwenda Kombe la Dunia Brazil. Kwa haraka haraka ndicho ambacho ninachokiona nikiona picha za Russia. Sura pekee zenye huzuni katika michuano ya Kombe la Dunia ni zile ambazo timu zao zimefungwa.

Vinginevyo, katika Kombe la Dunia kila mtu ana furaha. Watu mbalimbali kutoka katika mataifa 32 duniani wanapishana Russia wakiwa na furaha na kubadilishana mawazo kuhusu tamaduni za nchi zao.

Achana na watu wa mataifa 32 ambao nchi zao zinashiriki, kuna watu wengine wengi ambao nchi zao hazishiriki lakini wapo wamezamia katika michuano. Kwa mfano, Tanzania. Kuna Watanzania kibao wapo Russia kwa sasa wakati Taifa Stars haijulikani ilipo!

Russia ya sasa, kwa mujibu wa uzoefu wangu, kila mtu anatabasamu. Kila mtu ameshika glasi ya plastiki yenye kinywaji. Iwe bia, soda, pombe kali au vinginevyo. Mitaani kuna majiko ya nyama na vyakula. Maisha ni furaha. Mwanadamu anaishi mara moja tu.

Kama ilivyo Russia ndivyo ilivyokuwa Brazil na kwingineko ambako michuano ya Kombe la Dunia inafanyika. Mitaani kuna watu wengi hata katika mji ambao hauna mechi. Mashabiki wanaandaliwa eneo kubwa kama ilivyo Mnazi Mmoja au Leaders na kunakuwa na ‘screen’ kubwa ya kuonyesha mechi zinazochezwa miji mingine. Hata kama katika mji huo kuna mechi lakini bado eneo hilo linajaa.

Katika eneo hilo kila mtu anacheza muziki kwa mujibu wa nchi yake unavyochezwa. Glasi mkononi, tabasamu usoni, warembo kando yako. Lugha ni moja tu, soka. Lugha ya pili ni starehe. Dakika 90 za mechi zina maana ndogo kuliko mazingira ya maisha ya Kombe la Dunia. Nenda siku moja uone.

Mitaani, kundi moja linakwenda Magharibi, kundi jingine linawahi kituo cha treni Mashariki, kundi jingine ndio kwanza limeingia katika mji, labda mechi yao ipo keshokutwa. Walio katika jezi rasmi za nchi yao ni rahisi kuwagundua. Wanaimba, wanakata viuno. Usidhani kama na wao wanafahamina sana. Hapana. Wanajuana kwa sababu ya utaifa wao. Wala si ndugu.

Wengine unakutana nao wakiwa na jezi mbalimbali. Unashangaa unakutana na mtu amevaa jezi ya Cameroon lakini nchi yake haishiriki. Ni jambo la kawaida. Amenunua tiketi kwao kwa ajili ya kula maisha. Mzungu mwingine unamuuliza kwa shangwe anatokea nchi gani anakujibu “South Africa’. Naye yumo. Unamgeukia Mwarabu kando yako unadhani ametoka Iran au Saudi Arabia kwa vile nchi zao zilikuwa kwenye Kombe la Dunia lakini anakujibu kwa kifupi ‘Natoka Afghanistan’.

Wiki moja tu ya maisha yako usikose kwenda kutazama Kombe la Dunia. Hata kama hauna tiketi. Maisha matamu zaidi ya Kombe la Dunia yapo nje kuliko ndani. Na ukianza kwenda katika michuano hii hautaacha. Unagundua kuna dunia nyingine tamu tofauti na dunia unayoifahamu. Dunia iliyojaa shida, watu wenye hasira, foleni za magari, joto na watu waliokunja sura muda wote. Kombe la Dunia litakuondoa katika dunia hii.

Unatengeneza marafiki wapya pia. Unakutana na watu ambao wala hawajui kama nchi yako ipo Afrika Mashariki. Unakutana na watu ambao wamewahi kupita nchini kwako. Unashangaa wanaweza kukwambia kitu cha ajabu zaidi.

Mwaka 2014 nilikuwa katika mji wa Salvador pale Brazil kushuhudia mechi ya Chile na Uholanzi. Katika fukwe zao nikakutana na Wazungu wamevaa jezi zilizoandikwa TANZANIA. Nikashangaa. Nikawasogelea nikawaambiwa nimetoka Tanzania. Wakaanza kupiga kelele kwa furaha huku wakisema ‘Hatutaki Muungano’. Nikashangaa sana. baadaye nikagundua kuwa waliwahi kwenda Zanzibar kama watalii wakakutana na zengwe kutoka kwa baadhi ya watu ambao walikuwa hawautaki Muungano. Nikacheka sana.

Nenda Kombe la Dunia hata kama hauna tiketi. Dunia hailali. Kama ilivyo Russia kwa sasa. Unaweza kuamka saa nane usiku na kutembea mtaani ukipishana na makundi ya watu tu. Baa ziko wazi. Warembo wanakatiza mitaani. Ni wewe tu na maamuzi ya roho yako pamoja na pesa mfukoni.

Ukienda Kombe la Dunia hautaacha. Nawajua rafiki zangu waliokwenda Afrika Kusini, Brazil na sasa wapo Russia. Mungu akiendelea kuwapa pumzi najua watakwenda Qatar. Sijawahi kwenda Olimpiki lakini nadhani Kombe la Dunia ni kilele kinachowakutanisha watu wengi wa mataifa mbalimbali wenye furaha zaidi.

Maisha yanataka nini zaidi? Dakika moja tu ya uhai wako siku moja na wewe uwe mmoja kati ya watu wanaoshangilia kombe hilo katika nchi iliyoandaa.

Televisheni yako inadanganya. Mwanadamu anaishi mara moja tu. mwanafalsafa mahiri wa Kigiriki, Aristostle aliwahi kutuambia ‘Furaha inatokana na sisi wenyewe tunavyotaka’. Shauri yako!