In Summary
  • Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania imetoa wito kwa viongozi watakaochaguliwa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) kuhakikisha wanawasilisha taarifa za viongozi wote waliochaguliwa pamoja na mabadiliko ya katiba

 Dar es Salaam. Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amekipongeza Chama cha Wananchi (CUF) kwa kufanya mkutano wake mkuu kwa kufuata Katiba yao na matakwa ya sheria ya vyama vya siasa.

Nyahoza alitoa kauli hiyo, leo Alhamisi Machi 14, 2019 wakati akitoa salamu kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwenye mkutano mkuu wa CUF unaoendelea katika Hoteli ya Lekam, Dar es Salaam.

Amesema kwa siku tatu alizohudhuria mkutano huo, ameshuhudia namna demokrasia ilivyotawala katika chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar licha ya kupitia katika tafrani.

“Tangu juzi nipo katika mkutano huu, nimeshuhudia jinsi ulivyoendeshwa na uvumilivu,  wajumbe mmeendesha kwa mujibu wa katibu yenu na mmeitisha kwa kufuata taratibu zilizopo, tunapenda vyama viheshimu sheria,” amesema Nyahoza.

“Nawatakia kila la kheri na wale wanaoleta ‘figisu figisu’ ya kutofuata katiba yenu watashughulikiwa. Usipotii sheria shughuli yake utaiona tu,” amesema.

Nabu msajili huyo ametoa siku 14 kwa chama hicho kuhakikisha wanawasilisha ofisi za msajili wa vyama vya siasa mabadiliko yote ambayo wameyafanya.

Katika taarifa hizo ambazo Nyahoza amewataka kuwasilisha ni pamoja na ya viongozi waliochaguliwa ngazi ya taifa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri zaidi