In Summary

Ni kutokana na usajili wake kuonekana kuwa wa watu binafsi


Dodoma. Serikali imeandaa pendekezo la kubadilisha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuwa shirika la umma ili kuondoa utata uliopo wa wamiliki wa kampuni hiyo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 17, 2018  na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha

2018/19.

Amesema NARCO ambayo imeanzishwa kwa Sheria ya Kampuni Sura Namba 212 ina utata kwenye usajili wake.

Amesema nyaraka za mkataba zinaonyesha kuwa wanahisa ni Clement Kahama na Hippolitus Pamfili Njau ambao walisaini kwa vyeo vya meneja mkuu na katibu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Amesema nyaraka hizo zimeendelea kusomeka hivyo hadi sasa na hivyo kuifanya kampuni hiyo kuonekana kuwa ni mali ya watu binafsi .

“Kutokana na mkanganyiko huo wizara yangu imeandaa pendekezo la kuibadilisha NARCO kutoka kampuni kuwa shirika la umma ili kuondoa utata huo na kupanua wigo wa kutekeleza majukumu yake,”amesema.