In Summary

Anaendelea kushikiliwa polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo na kujiteka

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea kumshikilia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kujiteka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 13, 2018 Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.

Nondo alidaiwa kutoweka Machi 6, 2018 lakini alijisalimisha mikononi mwa polisi wilayani Mafinga, Iringa Machi 7.

Baada ya kujisalimisha alifunguliwa jalada la uchunguzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire ambaye aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo ni kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani.

Machi 10, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa litakapomalizana na Nondo limrejeshe jijini Dar es Salaam ili na yeye aanzishe uchunguzi wake kwa mwanafunzi huyo.