In Summary

Kisa cha mwanafunzi huyo kupigwa ni kushindwa  kuchonga mwiko

Musoma.  Mwalimu wa Shule ya Sekondari Ngoreme Wilaya ya Serengeti mkoani Mara anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo.

Akizungumza leo Mei 17, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki amesema mwalimu huyo alimshambulia kwa ngumi na makofi sehemu mbalimbali za mwili mwanafunzi wake, Michael Charles katika tukio lililotokea Mei 15, 2018.

“Tunaendelea na uchunguzi na tutamfikisha mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika,” amesema Kamanda Ndaki

Baada ya shambulio hilo, mwanafunzi huyo alikimbizwa Kituo cha Afya Iramba wilayani Serengeti kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara mjini Musoma alikolazwa kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na MCL Digital,  Michael amesema alipigwa na mwalimu wake kama sehemu ya adhabu baada ya yeye na wenzake kushindwa kutekeleza agizo la kuchonga mwiko wa kupikia.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Hosea Bisanda amesema madaktari hospitalini hapo wanaendelea kumhudumia mgonjwa huyo na kwamba hali yake imeanza kuimarika.