In Summary

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametangaza neema kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu wa lugha ya Kiswahili, akieleza kuwa Serikali inawahitaji kwenda katika balozi za Tanzania nchi mbalimbali duniani kufundisha lugha hiyo

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametangaza neema kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu wa lugha ya Kiswahili, akieleza kuwa Serikali inawahitaji kwenda katika balozi za Tanzania nchi mbalimbali duniani kufundisha lugha hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 11, 2019 wakati akikabidhi vyeti kwa wahitimu 136 wa ualimu wa Kiswahili waliopata mafunzo kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita).

Mwakyembe amesema lugha ya Kiswahili inakwenda kuwa lugha kubwa duniani na mataifa mengi yanahitaji walimu wa kufundisha lugha hiyo.

"Jiandaeni kwenda kufundisha lugha yetu ya Kiswahili duniani maana ni moja ya mkakati wa Serikali, naomba mkae mkao wa kula kama hamna hati za kusafiria  zitafuteni muda wowote tutawahitaji kwenda katika balozi zetu za Tanzania kufundisha Kiswahili,” amesema.

Mwakyembe amesema kati ya lugha 6,000 zinazozungumzwa duniani kuna lugha 10 ambazo zinazungumzwa sehemu nyingi, Kiswahili kipo na ifikapo mwaka 2060, Kiswahili itakuwa lugha ya utambulisho wa Mwafrika.

"Hivi karibuni Afrika Kusini imetutangazia inahitaji kuanza kufundisha Kiswahili katika masomo yao  kwa shule zote na Sudan pia wametangaza hivyo, jiandaeni mambo yanakwenda kuwa mazuri," amesema Mwakyembe.

Mwakyembe amesema kutokana na uhitaji huo wizara yake imeungana na wizara tatu; ya Elimu, Tamisemi na Mambo ya Nje kusaka njia ya kuzalisha walimu wa kutosha wa Kiswahili.

Katibu mtendaji wa Bakita, Seleman Sewange amesema hadi sasa baraza limepokea watu 576 wanaopata mafunzo hayo, 136 wametunukiwa vyeti leo.