In Summary

Kutokana na hali hiyo simba wameanza kutoka hifadhini

Arusha. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), limesitisha kwa muda watalii kuingia katika Hifadhi za Taifa ya Ziwa Manyara kutokana na miundombinu kuharibiwa na maji.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumanne, Aprili 17, Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete amesema mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha zimeharibu miundombinu katika hifadhi hiyo na kufanya vivutio kutofikika kwa urahisi.

Amesema daraja la Mto Marera lililopo kilomita moja kutoka lango la kuingia ndani ya hifadhi hiyo limechukuliwa na maji.

"Tunawasihi wageni wote waliopanga kutembelea hifadhi ya Manyara kuahirisha kwa muda," amesema.

Akizungumzia uharibifu wa miundombinu hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Ziwa Manyara, Noelia Myonga amesema kutokana na uharibifu wa maji hivi sasa ni vigumu kutembelea maeneo ya vivutio ndani ya hifadhi.

"Tangu asubuhi tunahangaika kurekebisha barabara na miundombinu mingine na tuna imani tutakamilisha kazi ili watalii waweze kuingia," amesema.

Amesema wamejaza mawe katika njia za kuingia hifadhini hasa kutokana na kujaa maji mito inayoingiza maji katika eneo hili ikiwepo mto Sasa na Endara.

"Tumejaza mawe, maji mto Sasa, pia eneo la  Endara kumejaa maji, eneo la Mabokoni, kumejaa pia maji na michanga," amesema.

"Tunawaomba watalii kuwa na subira kidogo tuna imani hali itakuwa nzuri," amesema

Kutokana na ongezeko kubwa la maji katika hifadhi ya ziwa hilo na eneo la ikolojia ya hifadhi ya Manyara na Tarangire, simba wameanza kutoka hifadhini .

Dume moja la simba leo limeonekana eneo la Makuyuni hatua ambayo sasa inatishia maisha ya watu.