In Summary

Vifo hivyo vimetokea juzi baada ya watu hao kuangukiwa na ukuta

Mkoani Tabora hali si shwari baada ya watu watatu kufariki na barabara ya Kaliua kwenda Kigoma na ya Tabora kwenda Mpanda zikiwa hazipitiki ipasavyo kutokana na madaraja kujaa maji.

Akizungumzia na MCL Digital leo Jumatatu, Aprili 16, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbrod Mutafungwa amesema Aprili 14 saa tisa usiku katika Kijiji cha Mirambo Wilaya ya Nzega watu watatu waliangukiwa na ukuta wa nyumba na kufariki dunia.

Kamanda Mutafungwa amesema watu hao walikuwa wakiishi katika nyumba ya tembe ambayo imejengwa kwa udongo kuanzia juu hadi chini.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Tatu Selemani(28), ambaye ndiyo alikuwa mama wa nyumba hiyo, Nasibu Majuto(4) na Selemani Kasuko(4).

Ameeleza kuwa mvua hizo zimesababisha adha kwa watumiaji wa barabara ya Kaliua kwenda Kigoma ambapo daraja la Kazilambwe limejaa maji kiasi yanapita juu ya barabara hivyo haitumiki kwa sasa.

Amelitaja eneo lingine lililojaa maji kuwa ni Mto Kogwa na kusababisha barabara ya Tabora-Mpanda kutopitika kutokana na mto huo kujaa maji hadi juu na kufunika barabara.