In Summary

Kwa mujibu wa dada wa Muna aitwaye Eve, msiba huo upo Mwananyamala kwa baba wa mtoto huyo.

 


Wakati watu wakisubiri kuupokea mwili wa mtoto wa Muna Love aliyefariki Julai 3, 2018 jijini Nairobi alikokuwa akitibiwa, dada wa msanii huyo amesema msiba uko kwa baba wa mtoto anayeishi Mwananyamala kwa Mwakibile jijini Dar es Salaam.

Mtoto huyo, Patrick alikuwa na uvimbe kichwani na wazazi wake kumpeleka Nairobi kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na MCL Digital, Eve, ambaye ni dada wa Muna, amesema wameamua kuweka msiba Mwananyamala kwa sababu ndiko nyumbani kwa baba yake.

“Msiba hauko huko Mbezi jamani. Patrick ana baba yake na yuko hai anaitwa Peter. Hivyo tuko hapa Mwananyamala kwa Mwakibile tunapanga jinsi ya kuurudisha mwili Tanzania kwa ajili ya maziko,ambayo tutawatajia siku,” alisema Eve.

Eve aliomba watu waachane na habari zinazosambazwa mitandaoni kuwa mtoto huyo ni wa mtangazaji maarufu wa televisheni, Caston, akisema ni za upotoshaji.

Amesema iwapo watu wanataka ukweli wa suala hilo, waende msibani kwa ajili ya kupata habari kamili.

“Kama nilivyokwambia mwanzoni, watu wasipende kuongea vitu ambavyo hawavijui. Ukweli ni kwamba Caston si baba wa Patrick kama inavyodaiwa,hivyo watu waachane na hizo habari za mitandaoni jamani,” alisema Eve.

Eve alisema Patrick ni mtoto wa mtu anayeitwa Peter ambaye ni mfanyabiashara.

Mbali na hilo, Eve pia alisema Patrick ameumwa kwa wiki mbili, kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kichwa uliosababishwa na uvimbe kichwani.

“Yaani mimi nimerudi jana tu kutoka Nairobi, huku nyuma napata habari Patrick amefariki. Imenuima sana, tulimpeleka Nairobi kwa ajili ya matibabu ya kichwa," alisema.

"Kichwa kilikuwa kinamuuma kila wakati, kilisababishwa na uvimbe kichwani, ila ndio hivyo Mungu amempenda Zaidi."

Mtoto huyo alipata umaarufu baada ya kuokoka akiwa na umri mdogo wakati huo alipata matatizo ya kusagika mfupa wa mguu wa kulia kabla ya kupona baada ya kutibiwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) mwaka juzi.

Umaarufu wa Patrick ulizidi baada ya kuanza kumshawishi mama yake kuokoka na kuachana na mambo ya kidunia.