In Summary

Kauli hiyo imetolewa bungeni na waziri wa maji, wakati akijibu maswali ya wabunge


Dodoma. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe amesema mpango mkubwa wa kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Dar es Salaam utaanza kutekelezwa mwaka ujao wa fedha mwaka 2018/19.

Waziri Kamwelwe ametoa ahadi hiyo leo Juni 13 bungeni 2018 wakati akijibu maswali mbalimbali ya wabunge.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi ameuliza katika maeneo ya Masaki, Tabata, Segerea, Oysterbay awali hakukuwa na maji lakini sasa yapo hata hivyo kuna maeneo mengine jijini Dar es Salaam bado yana uhaba wa maji.

Mbunge huyo akahoji je Serikali ina mpango gani wa kuyasaidia maeneno hayo? Akijibu swali hilo, Waziri Kamwelwe amesema: “Tumepata fedha Sh57 bilioni kutoka Benki ya Dunia na tumetangaza zabuni ya kusambaza maji katika jiji la Dar es Salaam na tutahakikisha maji yanapatikana maeneno yote ya Dar es Salaam.”

Mara baada ya jibu hilo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea akauliza: “Tatizo la maji limekuwa kubwa karibu majimbo yote na Serikali ni lini hasa mradi huu utaanza katika jiji la Dar es Salaam?”

Akijibu swali hilo la Kubenea, Waziri Kamwelwe amesema, “tunaanza mwaka ujao wa fedha kwani tumeshatangaza zabuni.”