In Summary

Adai ana taarifa kuna baadhi ya vyama vya siasa vimeweka kambi katika maeneo ya jiji hilo kwa ajili ya kufanya vurugu

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Albert Chalamila amewaonya watakaothubutu kuvuruga amani kuelelea Septemba 16 siku utakapofanyika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Chalamila alisema: “Watu wanaotaka kuipoteza amani katika mkoa wetu hatutawacha, tutawashughulikia kwani mikono yetu inawasha na  mtu wa kuikuna ni ambaye atavunja kanuni, sheria na mienendo ya Taifa letu.”

Chalamila alisema ana taarifa kuna  baadhi ya vyama vya siasa vimeweka kambi katika maeneo ya jiji hilo kwa ajili ya kufanya vurugu na kuvitaka vikundi hivyo kusambaratika.

Alisema siku ya uchaguzi hatarajii kuona wananchi wakiwa wamevalia sare za vyama vya siasa na kubeba bendera na kuwataka kutokaa karibu na vituo vya kupigia kura mara baada ya kupigaji kura kuchagua viongozi wanaowataka.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimeanzisha utaratibu maalumu utakaokuwa endelevu wa kufanya mazoezi katikati la jiji la Mbeya na maeneo ya pembezoni kwa ajili ya kujiimarisha na kufanya usafi.

“Ninaomba niwatoe hofu wakazi wa Mbeya wakiona wanajeshi, FFU (Kikosi cha Kutuliza Ghasia), magereza na askari polisi wakizunguka maeneo yao wasishtuke na kuhamaki kwani watakua kwenye kazi maalumu,” alisema Chalamila.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema polisi kwa kushirikiana na wadau wa ulinzi na usalama wamejipanga kukahikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu.

Alisema watahakikisha kuwa uchaguzi huo utakuwa wa haki na hakutawa na vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Mbeya tuna magari na polisi wa kutosha ambao watadhibiti uvunjifu wa amani ambao unaweza kujitokeza wakati wa uchaguzi,” alisema.