In Summary

Mgombea ubunge wa CUF jimbo la Ukonga, Salama Omary amesema wananchi wakimchagua kuwa mwakilishi wao bungeni,  atahakikisha wanapata ajira, kuwaboreshea huduma za afya na kuinua uchumi kwa vijana

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa CUF jimbo la Ukonga, Salama Omary amesema wananchi wakimchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, atahakikisha wanapata ajira, kuboresha huduma za afya, kuinua uchumi kwa vijana.

Akizungumza leo Ijumaa Septemba 14, 2018 katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Nyanza Kitunda, Salama  amesema chini ya uongozi wake katika jimbo hilo, watoto chini ya miaka mitano, akina mama na wazee watatibiwa bure.

Amesema katika kuinua uchumi atawashawishi wafanyabiashara wakubwa, akiwemo Salim Bakhressa kuwekeza katika jimbo hilo.

“Naombeni mnichague maana mimi ni mtu mwenye huruma. Tutahakikisha huduma za afya zinatolewa bure kwa akinamama, wazee na watoto kupitia fedha za mfuko wa jimbo,” amesema.

“Mkinichagua nitahakikisha ninainua uchumi kwa vijana na kuwapatia ajira kupitia wawekezaji. Nitatafuta wawekezaji kuja kufanya uwekezaji hapa, najua wana Ukonga ni wazalishaji wa matunda nitamshawishi Bakhressa kuja kuwekeza kiwanda cha matunda hapa.”

Amesema, “endapo wananchi mtanichagua nitahakikisha naboresha elimu kwani wanafunzi wa Ukonga wanasoma katika mazingira magumu, shule nyingi hazina mabweni na vyumba vya madarasa havitoshi.”

Kuhusu miundombinu, amesema barabara za jimbo hilo ni mbovu na atakachofanya ni kuishawishi Serikali ili barabara hizo zikarabatiwe.