In Summary

Ni katika banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na inaelezwa kuwa ameletwa mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha ufugaji.


Dar es Salaam. Najua unamfahamu jogoo. Lakini huyu anaitwa Silk na anaweza kuwa wa kipekee kidogo.

MCL Digital imemkuta jogoo huyu leo Julai 5 katika maonyesho ya 42 ya kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba na kuelezwa kuwa anauzwa kwa bei ya Sh 800,000.

Ni katika banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na inaelezwa kuwa ameletwa mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha ufugaji.

 Jogoo huyo aliyepewa jina la Silk, hana tofauti na jogoo wengine, ni wa kisasa, ana kilo tatu, ana umri wa miezi sita lakini ana manyoya marefu na yaliyojipanga vizuri ukilinganisha na kuku wengine.

Akizungumza katika banda la JKT anayemtunza jogoo huyo Joshua Buberwa alisema jogoo huyo anapatikana nchini Malaysia na amechukuliwa na JKT kuja nchini ili kuwaonesha wananchi fursa mbalimbali zilizopo katika ufugaji.

“Kwa JKT bado hatujaanza rasmi kumfuga, amekuja katika maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kumtambulisha  na hatujaleta wengi ili kama watu watakaompenda wataagiziwe," 

Amesema katika banda la JKT wapo kuku wa aina mbalimbali lakini huyo aMEvutia wengi.

Buberwa amesema jogoo huyo ni kwa ajili ya mapambo na watalii ndiyo maana hata bei yake ni kubwa.

“Mwananchi wa kawaida anaweza kushangaa bei, lakini mtalii hawezi kwa sababu anajua ni wa mapambo,” amesema

"Ukitaka kumla unamla hana neno na ana nyama kama kuku wengine isipokuwa tofauti yake ni kuwa na manyoya mengi na laini,"amesema.

Amesema anafugwa kama kuku wa kizungu kwa kupewa chanjo kila mara kwa sababu ni rahisi kushambuliwa na magonjwa.