In Summary

Mshtakiwa huyo alikana kosa huku upande wa mashtaka ukidai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, meneja wa soko la wafanyabiashara wadogo la Machinga Complex lililoko jijini Dar es Salaam, Nyamsukura Masondore kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Akimsomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sophia Gura alidai kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Septemba 29 na Oktoba 7, 2014 akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Gura alidai kuwa Masondore akiwa na jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za jengo hilo, kwa makusudi alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa eneo ambalo halijaidhinishwa kwenye jengo hilo kwa Umoja wa Wauza Mitumba.

Alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume na kanuni namba 12 (a) na (b) za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa kutokana na kitendo hicho, mshtakiwa Masondore alijipatia faida yeye pamoja na wengine.

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alikana kosa huku upande wa mashtaka ukidai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Hata hivyo, wakili anayemtetea, Jamhuri Johnson ameiomba Mahakama impatie dhamana mteja wake huyo na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi.

Hakimu Sachore alitoa masharti ya dhamana akimtaka Masondore kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho kutoka katika taasisi zinazotambulika kisheria na wasaini ahadi ya Sh5 milioni.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 20 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Hadi jana saa tisa alasiri mshtakiwa huyo alikuwa bado hajakamilisha masharti hayo ya dhamana.