In Summary

Mbunge huyo ameilaumu Serikali kwa kukosa nia ya dhati katika kuinua kilimo.


Dodoma. Mbunge wa Singida Kaskazini, Justine Monko amesema Tanzania inakosa nia ya dhati katika kuinua kilimo ikiwemo kushindwa kutenga fedha kwa ajili ya kufufua zao la alizeti.

Monko amesema hadi sasa Serikali inatumia zaidi ya Sh413 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta ghafi kutoka nje wakati ingekubali ushauri wa wabunge fedha hizo zingetumika kuwekeza kwa wakulima wa alizeti na kutosheleza mahitaji na kuajiri watu wengi.

Amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi vijijini wanategemea shughuli za kilimo lakini hawajasaidiwa kikamilifu na serikali na hivyo kuwafanya wabaki katika hali ya umasikini mkubwa wakati ukuaji wa sekta ya kilimo unakwenda kwa kasi ndogo.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Fatuma Tawfiq alimesema katika hotuba nzima ya bajeti hiyo hakuna mahali Waziri amegusia kuhusu kilimo cha zabibu wakati ndiyo zao pekee kwa mkoa wa Dodoma hivyo akabainisha hotuba hiyo ni kama imeuacha mkoa wa Dodoma.

Tawfiq amezungumzia pia zao la alizeti kwamba pamoja na kuonekana kuwa ni mkombozi kwa wakulima, lakini bado zao hilo linakabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya ukosefu wa mbegu bora kwa wakulima.

Ameitaka wizara hiyo kujipanga na kuwekeza katika zao hilo kwa mambo mengi ambayo yatasaidia kuliboresha ili wakulima wafurahie kilimo hicho.

Mbunge wa Nkasi Kusini Deosdelisi Mipata amesema mipango ya kilimo ndani ya Serikali ni mibovo ambayo inashindwa kuwapeleka mbele wakulima.

Mipata amesema zao la mahindi kwa mkoa wa Rukwa linalimwa kwa asilimia 43 ya mazao yote yanayolimwa huko lakini tija yake bado ni ndogo sana.

“Naomba Serikali ibadilike kimtazamo katika kilimo, hivi sasa kilimo si kile kilichokuwepo huko nyuma na katika maeneo mengi lazima tubadilike na kuacha mazoea,” amesema Mipata.