In Summary
  • Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) Ally Keissy amekerwa na matumizi ya fedha za kigeni kutumika kununulia vitu visivyo vya muhimu

Dodoma. Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) Ally Keissy amekerwa na fedha za kigeni kutumika kununulia vitu vya ajabu ajabu ikiwemo kucha na kope.

Akichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2019/20, bungeni leo Ijumaa Novemba 9, 2018, Keissy amesema wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere fedha za kigeni zilikuwa zikitumika kununulia vitu muhimu.

“Tunapoteza hela za kigeni, tunaagiza vitu vya ajabu ajabu mpaka leo ukienda madukani unakuta mchele wa kihindi upo. Wakati mchele umejaa nchi nzima. Vitu vya anasa tunaagiza hadi kope mpaka kucha enzi ya Mwalimu Nyerere nakumbuka tulikuwa tunaagiza vitu vya muhimu,” amesema.

Amesema Tanzania imekuwa ikiuza mazao kama pamba na korosho kwa ajili ya kupata fedha za kigeni lakini watu wanaenda China kuagiza vitu vya ajabu ajabu na hivyo kukosa udhibiti wa dola.

Amesema fedha ya Tanzania imekuwa inaanguka kila siku kwa sababu ya uagizaji wa  vitu vya ajabu ajabu, vingine ni bidhaa feki na kutoa mfano wa juzi akiwa Dodoma ameshuhudia kofia ya bodaboda iliyoanguka ikivunjika.