In Summary
  • Wabunge wameendelea kumtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kujirekebisha kwa kauli anazozitoa wakati akitekeleza wajibu wake

Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaack Kamwelwe ameendelea kuandamwa na wabunge kuhusu majibu anayotoa kwa wabunge wanapomuuliza kuhusu mambo mbalimbali.

Baadhi ya wabunge waliolalamikia majibu ya Kamwele ni Ramadhan Dau (Mafia-CCM), Seleman Bungara (Kilwa Kusini-CUF) na leo Ijumaa Novemba 9, 2018 wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20  Mbunge wa Rufiji (CCM) Mohamed Mchengerwa naye amemtaka kujirekebisha na kurejea katika kasi aliyokuwa nayo wakati akiwa Waziri wa Maji.

“Sisi ni miongoni mwa watu ambao tulimpongeza sana wakati akiwa Waziri wa Maji lakini amekuwa akitoa kauli wakati fulani ambazo haziridhishi,” amesema na kuongeza:

“Nichukue nafasi hii kumweleza ile kazi nzuri aliyoifanya wakati akiwa Waziri wa Maji basi aiendeleze yapo maeneo ambayo mheshimiwa Rais aliweka ahadi ambazo ni sheria zinazohitaji kutekelezwa lakini wewe mheshimiwa waziri ukinijibu kuwa ulioachiwa na Profesa (Makame) Mbarawa huhusiani nayo napata tabu sana.”

Amesema majibu hayo yanamfanya apate tabu sana kumwelewa anawasaidiaje wananchi na kwamba sheria ya uongozi inawataka viongozi kugusa mioyo ya watu wao na wenyewe.

“Nimuombe mheshimiwa waziri arekebishe na arejee katika kasi yake nzuri aliyokuwa nayo wakati akiwa waziri wa maji,” amesema.