In Summary

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema anatamani chama hicho kikuu cha upinzani nchini kiongoze nchi, huku Watanzania wakiwa matajiri na si masikini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema anatamani chama hicho kikuu cha upinzani kiongoze nchi, huku Watanzania wakiwa matajiri na si masikini.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Ukonga, Asia Msangi.

Amesema Rais John Magufuli amekuwa akitamka kuwa ni kiongozi wa wanyonge, kwamba wananchi ni masikini

“Natamani siku moja chama changu kiongoze nchi hii watu wakiwa matajiri au kuna anayetaka umaskini,” alihoji Mbowe na kujibiwa na wananchi, “hapana.”

Amesema wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, maisha hayakuwa magumu lakini katika Awamu ya Tano, hali imebadilika na maisha yamekuwa magumu kwa maelezo kuwa bidhaa zimepanda bei.

Amedai kuwa umasikini sasa umeongezeka kwa ajili ya biashara ya kuwanunua viongozi na wabunge wa upinzani, kusababisha kuwepo na chaguzi za mara kwa mara za marudio.

“Watanzania tukiendelea kufumbia macho biashara inayofanyika na marudio ya hizi chaguzi tutaendelea kuwa maskini na hatutakuwa na maendeleo yoyote,” amesema.