In Summary

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amemjibu mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara aliyedai kuwa alikihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa kuwa nia yake ya kugombea uenyekiti iligeuka shubiri

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amemjibu mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ukonga, Mwita Waitara aliyedai kuwa alikihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa kuwa nia yake ya kugombea uenyekiti iligeuka shubiri.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Asia Msangi.

Waitara alikuwa mbunge wa Ukonga, alihama Chadema  na kujiunga na CCM ambako amepitishwa tena kuwania ubunge.

Wakati akieleza uamuzi wake wa kujiuzulu Julai 28, 2018, Waitara alisema umetokana na kuhoji suala la matumizi ya ruzuku na hoja yake ya kutaka mwenyekiti wa Chadema awe anabadilika, ambayo alidai ilifanya achukiwe na Mbowe.

Lakini leo katika mkutano huo wa kampeni, Mbowe amewataka wananchi kumpuuza Waitara aliyedai kuwa pia amekuwa akimhusisha na shambulio la kupigwa risasi la mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mbowe amesema wanaohusika na tukio la Lissu kupigwa risasi wanatambulika  na ndio sababu hadi sasa uchunguzi haujafanyika.

“Kama kweli Mbowe anahusika kwanini asikamatwe badala yake wamekuwa wakinitukana. Puuzeni maneno ya Waitara. Ameacha ubunge mwenyewe kwa kununuliwa,  leo hana hoja ya kuja kwenu,” amesema Mbowe.

“Mimi nimelala gereza la Segerea,  nimelala gereza la Ukonga niwambieni tu kule ni nyumbani kwenu tuache uoga na Jumapili tuonye tunataka Tanzania mpya.”