In Summary

Utafiti umeonyesha matokeo chanya katika kuzuia mbu kuingia ndani kwa asilimia 75 na asilimia 20 wasiambukize malaria

Dar es Salaam. Taasisi ya Afya Ifakara (IhI), imetoa matokeo ya utafiti wa majaribio wa namna ya kukabiliana na mbu wanaoeneza malaria kwenye makazi ya watu.

Matokeo hayo yametolewa leo na mkuu wa mradi wa utafiti huo, Dk Ladslaus Mnyone katika halfa iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubiysa na Shirika la Maendeleo la Watu la Uingereza (HDIF) ambao ni wafadhili wa utafiti huo.

Akitangaza matokeo hayo, Dk Mnyone alisema utafiti huo umeonyesha matokeo chanya katika kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba kwa asilimia 75, huku asilimia 20 ikiwezekana kuzuia watu wasiambukizwe  malaria.

Alisema utafiti huo umefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayoitwa ‘tunguli bomba’ zinazofungwa kitaalamu katikati ya paa na ukuta kwenye nyumba ya mtu.

Alisema ndani ya tunguli bomba kuna chandarua maalumu kilichowekwa kiatilifu chenye unga kinachosaidia kuwadhibiti mbu wasiingie ndani ya nyumba sambamba na kufariki dunia baada ya kunusu dawa hiyo.

“Kulingana na tafiti na uelewa uliotengenezwa kwa takribani karne moja iliyopita, mbu wanaoeneza malaria  kwa kiasi kikubwa wanaingia ndani ya nyumba kwa kupitia uwazi uliopo kati ya paa na ukuta ambao kwa kiswahili fasaha unaitwa ‘tungulizi’.

“Mbu hawa wanapenda kuingia kupitia eneo hilo kwa sababu mtu anapolala huwa anatoa hewa ambayo ni kivutio kwa mdudu huyu na hewa hii ikiongezaka hadi kufikia kiwango cha paa na ikafika sehemu rahisi ya kutokea ni tungulizi, ndiyo maana utafiti wetu ulilenga sehemu hii,” alisema Dk Mnyone.

Kwa upande wake, Dk Ulisubisya alisema Tanzania ni kati ya nchi 10 duniani zenye  zinazoathiriwa zaidi na malaria na kilahatua yenye nia kupunguza na kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini itapokelewa kwa mikono miwili.

“Wote tunafahamu malaria inapatikana pale ambapo mbu wameruhusiwa kuzaliana kwa urahisi na wakatuuma nje au ndani ya nyumba zetu. Imani yetu kila mbu anayekuja anakuja na ugonjwa kwa sababu hatuna macho ya utaalamu ya kubaini wasiokuwa na vijidudu.”

“Ndani ya nyumba zetu lazima tuweke mazingira ambayo hata mbu akiingia hadumu. Matumaini yetu Serikali ya Uingeza itahakikisha mbinu hii itakuwa rahisi  wananchi wetu wapate na kufunga katika nyumba zao ili kudhibiti malaria,” alisema Dk Ulisubisya.