In Summary
  • Katika mazishi ya mtoto huyo ambaye alifia hospitali baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kukatwa koromeo, simulizi ya mama aliyemwokoa baada ya tukio hilo pamoja na mama mzazi wa mtoto huyo, zilizidisha majonzi kwa waombolezaji.

Njombe. Vilio na majonzi jana yalitawala katika mazishi ya mtoto Meshack Myonga (4) ambaye alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata baada ya kutekwa kisha kukatwa koromeo na watu wasiojulikana.

Katika mazishi ya mtoto huyo yaliyofanyika kijijini kwao Ngalanga, Kata ya Iwungilo wilayani Njombe na kuhudhuriwa na umati wa watu, simulizi za mama aliyemwokoa mtoto huyo baada ya kukatwa koromeo na mama mzazi zilizidisha majonzi kwa waombolezaji.

Mtoto huyo ambaye alikuwa mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema, Njombe alitekwa na mtu asiyejulikana Desemba 23 mwaka jana akiwa nyumbani kwao muda mfupi baada ya kuachana na mama yake, Rabia Mlelwa.

Meshack alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya alikopelekwa kuchunguzwa maendeleo ya kidonda chake baada ya kuruhusiwa Januari 19 kurudi nyumbani.

Akisimulia, mkazi wa Mji Mwema, Jane Chanda ambaye alimbeba mtoto huyo kutoka eneo la tukio hadi hospitalini alisema alikuwa shuhuda wa pili kumuona mtoto huyo akitanguliwa na kijana mmoja ambaye alimuona mtoto huyo akitokea msituni akikimbilia barabarani eneo la Kanisa la Lutherani-Mji Mwema.

“Yule kijana wakati anapita eneo lile alimuona mtoto Meshack akijirusha kutoka msituni akiwa uchi na mkononi akiwa ameshika sweta, nilipomuuliza umemtoa wapi huyu mtoto ndipo akaniambia nimemuona akitokea msituni huku.”

“Basi mimi nikasema tukatoe taarifa kwa balozi, lakini wakati huo mtoto akiwa uchi kabisa huku akionekana kukatwa shingoni,” alisimulia.

Alisema baada ya hapo alimfunga na kanga yake kisha kumpeleka zahanati na walipofika hapo ikaonekana anahitaji matibabu makubwa hivyo wakaondoka na balozi kwenda Hospitali ya Mkoani ya Kibena.

“Wakati nawaona na kijana yule, mtoto alikuwa anatembea na hata msituni kwenda barabarani alikuwa anatembea mwenyewe lakini alikuwa haongei na damu zikivunja kwa wingi,” alisema.

Alisema hadi wanafika Hospitali ya Kibena Meshack alikuwa anajitambua licha ya kushindwa kuzungumza, lakini alianza kupoteza fahamu wakiwa njiani kuelekea Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Alisema kwa vile mtoto huyo alikuwa hafahamiki ni wa nani, alisema alilazimika kumhudumia hadi hospitalini Mbeya.

“Tulifika Mbeya, saa 12 jioni, wakampatia huduma, wakamshona nyuzi kwenye koromeo huku akiwa amezirai na ilipofika saa sita usiku alizinduka.

“Akaanza kuzungumza, nikaanza kumuuliza jina lako, akaniambia jina lake na anakokaa hapo nikaanza kupata picha halisi ya wazazi wake wanakaa wapi,” alisema.

Alisema siku ya pili, wazazi wake walifika na siku ya tatu alirudi Njombe na akamuacha mama yake akiendelea kumhudumia.

“Nilimuacha mtoto akiwa hali ya kupona kabisa. Hata niliporudi niliendelea kuwasiliana naye na hata waliporudi nilikwenda kuwaona. Mtoto alikuwa amepona kabisa alikuwa anazungumza, anakula chakula mwenyewe.

Mama wa mtoto huyo, Rabia Mlelwa alisema baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini Januari 19, aliambiwa arudi Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kuangalia maendeleo yake na kumtoa nyuzi.

Alisema kwanza walipelekwa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Njombe na juzi Jumamosi ndipo alipopokewa na kuingizwa chumba maalumu.

“Asubuhi tulikwenda mtoto akapelekwa chumba maalumu, ilipofika mchana wa saa nane niliitwa na madaktari na kunipa taarifa kwamba mwanangu amefariki. Hata sielewi imekuwaje huko ndani hadi mwanangu afariki.

“Wakaniambia mwanangu koromeo lake lilikuwa limesinyaa na kwa ndani damu ilikuwa inavuja, hivyo alikuwa mtu wa kufa muda wowote ule.”

Akizungumza kwenye mazishi hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Emmanuel George alisema Serikali haitanyamazia matukio hayo na wote wanaohusika lazima wasakwe popote walipo.

“Serikali ipo macho, haitalala, tunaendelea kuchukua hatua, naombeni wananchi mtoe ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kila hatua,” alisema.

Diwani wa Iwungilo, Reginald Danda aliwataka wananchi kutoa taarifa za wageni wote wanaofika kwenye nyumba zao kwa viongozi wa Serikali ili kutambuana.

“Niwaombe sana ndugu zangu katika kipindi hiki kigumu tuwe na uangalifu mkubwa mno. Kuna wageni wanaingia na kutoka na sio wote wenye uwezo kujieleza mkamuelewa harakaharaka, hivyo msione akibabaika kujieleza mkachukua sheria mkononi na mkatenda kosa kwa raia mwema, mtu kama huyo mpelekeni ofisini kwa hatua nyingine zaidi,” alisema