In Summary

Akizungumzia maadhimisho ya siku ya vijana duniani yatakayofanyika jijini Arusha, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Antony Mavunde alisema jana kuwa walianza na kubadilisha mtazamo kuhusu kilimo.

Dodoma. Serikali imetangaza mikakati minne mikubwa ambayo itasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana ikiwemo kuanzisha programu maalumu ya kuwafundisha jinsi ya kutengeneza vitalu nyumba (green house).

Akizungumzia maadhimisho ya siku ya vijana duniani yatakayofanyika jijini Arusha, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Antony Mavunde alisema jana kuwa walianza na kubadilisha mtazamo kuhusu kilimo.

“Na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana,” alisema Mavunde.

Alisema mkakati mwingine ni kutenga maeneo maalumu ambapo hadi sasa wametenga hekta 217,000 ili vijana wanaomaliza masomo wakitamani kujishughulisha na kilimo wawe na maeneo.

Alitaja eneo jingine kuwa ni uwezeshaji ambalo linatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, ambapo wamekuwa wakiwaunganisha na mifuko ya uwezeshaji wa kiuchumi nchini inayotoa ruzuku na mikopo.

Alisema pia wako mbioni kuanzisha programu ya kitalu nyumba (green house) ambapo wataanza vijana 3,500 kutoka katika wilaya 35 kwenye mikoa mitano.

“Watafundishwa kutengeneza green house nao pia wakafundishe wengine. Lakini pia tutawatengenezea green house,” alisema naibu waziri huyo.

Akielezea kuhusu maadhimisho hayo, Mavunde alisema Agosti 10, vijana watafanya shughuli za kujitolea kwa kupanda miti katika Chuo cha Polisi Tengeru na Hospitali ya Wilaya Meru mkoani Arusha.

Alisema pia kutafanyika tamasha la afya ya uzazi katika Kituo cha Mabasi Tengeru na Agosti 11 kutakuwa na kongamano litakalowashirikisha vijana na wadau katika ukumbi wa mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Agosti 12 kutafanyika tamasha katika Chuo cha Ualimu cha Patandi, Tengeru ambalo litahusisha maandamano ya amani. Lakini pia kutakuwa na maonyesho ya kazi ya wadau wa maendeleo ya vijana,” alisema.

Mmoja wa wadau wa vijana, Aminiel Mongi alisema maadhimisho hayo ni mazuri na hasa kwa sababu moja ya malengo ni kuwawekea mazingira mazuri kiafya ili waweze kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi.