In Summary

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ameongeza hisa zake katika kampuni ya Fastjet Tanzania kutoka asilimia nne za awali mpaka 68


Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ameongeza hisa zake katika kampuni ya Fastjet Tanzania kutoka asilimia nne za awali mpaka 68.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mpango wake wa kununua hisa zote kutoka kampuni mama ya Fastjet PLC ya Afrika Kusini ili kampuni hiyo ya ndege imilikiwe na Watanzania.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 6, 2018, Masha ambaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti mtendaji wa Fastjet Tanzania, amesema wiki iliyopita alinunua asilimia 47 ya hisa za kampuni hiyo zilizokuwa zikimilikiwa na wazawa na asilimia 17 za kampuni ya Fastjet PLC.

Kwa uamuzi wake huo, kwa sasa ndiye mwenye hisa nyingi za kampuni hiyo, ukiacha asilimia 32 ya hisa zinazobaki ambazo zinamilikiwa na raia wa Afrika Kusini, Hein Kaiser.

Mpango wa kununua hisa zote na kuifanya Fastjet Tanzania kuwa kampuni ya Kitanzania ulikuja baada kampuni ya Fastjet PLC kutangaza kwamba ingesitisha mara moja kutoa fedha kwa kampuni ya Fastjet Tanzania.

Hata hivyo, ofisa uhusiano na masoko wa kampuni ya Fastjet Tanzania, Lucy Mbogoro amesema kampuni hiyo inatafuta wawekezaji wa kimkakati.

Fastjet PLC ni kampuni ya ndege ya Uingereza/Afrika Kusini inayofanya usafirishaji ndani ya Bara la Afrika. Kampuni ilibainisha lengo lake la kuwa kampuni ya ndege inayotoa huduma kwa gharama ndogo zaidi Afrika.

Uendeshaji wa kampuni hiyo ulianza kwa kutumia jina la Fly540 na nchini ilianza safari zake Novemba 2012.