In Summary

Wachezaji wa timu ya Borussia Dortmund wanaamini kuwa wanapaswa kubeba lawama kutokana na kipigo cha mabao 2-0 walichokipata kutoka kwa Atletico Madrid, katika Ligi ya Mabingwa Afrika.  


Munich, Ujerumani. Mshambuliaji nguli wa Borussia Dortmund, Mario Goetze, amewaambia wachezaji wenzake kupuuza kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico Madrid na kuelekeza akili na nguvu zao dhidi ya Bayern Munich Jumamosi hii.

Kipigo hicho kutoka kwa Atletico kilikuwa cha kwanza kwa Dortmund msimu huu wa 2018/19 na Goetze anaamini lawama lazimi zibebwe na wachezaji wenyewe.

Hadi hivi sasa Dortmund inaongoza Ligi kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya bingwa mtetezi Bayern Munich ambayo msimu huu haina makali yaliyozoeleka.

"Kupoteza mchezo wetu kutoka kwa Atletico kutapaswa kuwa somo kwetu, tulifanya makossa mengi katika mchezo huo, lakini hatupaswi kukata tamaa, badala yake tujipange dhidi ya Bayern Munich.

Katika mchezo huo kipa wa Dortmund, Roman Buerki, ambaye alikuwa amefungwa mabao kumi pekee msimu huu, alisema anaamini kipigo hicho kitawazindua wachezaji wote.

"Kwa hakika kipigo hichi kutoka kwa Atletico hakitakuwa kibaya sana kwetu bali kitakuwa sababu ya kuzinduka, wakati mwingine kosa moja huwa sababu ya kujinusuru kwa mambo kadhaa,” alisema Buerki.

Naye nahodha wa klabu hiyo Marco Reus, ambaye msimu huu yupo katika kiwango bora akifunga mabao tisa na kupika saba katika mechi 16 alizocheza kwa mashindano mbali mbali msimu huu, alisema wanakipuuza kipigo hicho.

Nahodha huyo alisema kuwa, wataingia kwenye dimba la nyumbani wikiendi hii kuhakikisha wanalipiza kisasi cha kufungwa mabao 6-0 na Bayern Munich katika mechi ya ugenini iliyochezwa Machi mwaka huu.