In Summary

Manchester United imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuilaza Juventus mabao 2-1 mjini Turin, jana usiku.


Turin, Italia. Manchester United imelipa kisasi dhidi ya ‘Kibibi Kizee’ cha Turin Juventus, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Man United ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Allianz mjini Turin, ilipata mabao mawili ndani ya dakika tano za mwisho.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Old Trafford, Man United ilichapwa bao 1-0.

Mabao ya kiungo wa pembeni Juan Mata alilofunga kwa mpira wa adhabu dakika ya 86 liliamsha morali ya wachezaji wa Man United ambao walishambulia lango la Juventus kama nyuki.

Presha hiyo ilisabanisha mchezaji wa Juventus Alex Sandro kuweka mpira kambani dakika ya 90 na kuamsha shangwe ya mashabiki wa Man United.

Sandro alijifunga kutokana na shuti la Ashley Young. Man United imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya 16 bora.

Awali, mshambuliaji wa zamani wa Man United, Cristiano Ronaldo alianza kutoa presha, baada ya kufunga bao kwa kiki kali iliyomshinda kipa David de Gea.

Licha ya kufungwa, Juventus inaongoza katika msimamo wa Kundi H ikiwa na pointi tisa, Man United saba, Valencia tano na Young Boys moja.