In Summary

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015

Dar es Salaam. Edward Lowassa aliyewahi kuelezewa na Tundu Lissu kama “tembo wa siasa za Tanzania” ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya mambo magumu katika kipindi ambacho hakikutarajiwa na wengi.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, katika ngwe yake ya kisiasa, amefanya mambo makubwa matatu ambayo yamekuwa yakizua mijadala ndani na nje ya vyama vyake.

Baadhi ya hatua ambazo amekuwa akichukua zimekuwa zikitikisa ndani na nje ya nchi, kuwaacha vinywa wazi washindani na wafuasi wake huku mwenyewe akiwa kimya au kusimamia kile alichokifanya.

Tukio la Jumanne wiki hii la kukutana na Rais John Magufuli na kufanya mazungumzo Ikulu na baada ya hapo mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema kuimwagia sifa Serikali, ni moja ya matukio ambayo hayakutarajiwa.

“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza naye na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo,” alisema Lowassa mbele ya Rais Magufuli.

Huu ni uamuzi mkubwa wa tatu wa Lowassa alioufanya katika kipindi chake cha siasa ambao umezua sintofahamu kuhusu hatima yake kisiasa ndani ya Chadema huku baadhi ya wana CCM wakimpongeza na kusema siasa si uadui.

Sifa hizo kwa Serikali ya CCM zimemuweka mbunge huyo wa zamani wa Monduli katika hali sintofahamu ndani ya Chadema, baadhi ya walitangaza hadharani kukerwa na kujitenga na kauli hilo huko baadhi wakitaka achukuliwe hatua za kinidhamu.

Tukio la pili ni lile lililotokea Julai 28, 2015 wakati Lowassa alipotangaza kukihama chama kilichomkuza kisiasa cha CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema baada ya jina lake kukatwa kwenye mchakato wa kupata mgombea urais ndani ya CCM.

Akitangaza uamuzi huo katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Lowassa alisema ‘’CCM si baba yangu wala mama yangu, Watanzania kama wameyakosa mabadiliko ndani ya CCM, basi watayapata nje ya CCM.”

Alisema hakukurupuka kuchukua uamuzi huo na kama angeendelea kukaa ndani ya CCM ingekuwa ni unafiki, “Sikukurupuka kuchukua uamuzi huu hivyo basi kuanzia leo (Julai 28, 2015) natangaza rasmi kuondoka CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema.”

Ni uamuzi ambao uliweka historia za siasa za Tanzania tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa mwaka 1992 kwa kiongozi aliyewahi kushika wadhifa wa juu kama Waziri Mkuu kuhama chama tawala na kwenda upinzani.

Tukio la tatu na kubwa kwa Lowassa ni lile la Februari 7, 2008 alipotangaza kujiuzulu uwaziri mkuu ikiwa ni miaka miwili tangu Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alipomteua katika awamu yake ya kwanza ya utawala wake.

Kujiuzulu kwa Lowassa kulitokana na kashfa kubwa iliyotikisa nchi ya Richmond ambayo ilitokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo, ambazo baadaye baadhi yake zilidaiwa kukiuka taratibu na sheria.

Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na kamati ya Bunge na taarifa yake kutolewa bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, Lowassa alilazimika kujiuzulu.Katika taarifa hiyo, Dk Mwakyembe alimtaka Lowassa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.

Lakini hakuwa Lowassa pekee aliyeng’oka madarakani, pia mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha waliachia ngazi.

Akizungumzia matukio hayo yaliyomsibu Lowassa, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dk Charles Kitima alisema ni mmoja wa wanasiasa ambao wako tayari kuwajibika pale inapobidi kulinda masilahi ya wananchi na Taifa.

“Ni mtu ambaye yuko tayari kuwajibika lakini kuwe na msingi wa kuwajibika. Mwaka 2008 aliombwa kujiuzulu uwaziri mkuu akakubali, kuheshimu matakwa ya watu na chama chake, unapoona wananchi wanataka tofauti, naye anafanya,” alisema.

Kuhusu kuhama chama, Dk Kitima aliyepata kuwa makamu mkuu wa Saut alisema, “Aliona anaweza kusaidia chama kingine na kwenda kumsalimia Rais aliona kunahitajika mazungumzo, hatuwezi kuendesha nchi bila kusikilizana.”

Hata hivyo, alisema kosa alilolifanya ni kutokuonyesha kasoro zilizopo katika utawala wake ambazo wananchi wanaona haziendi sawa katika maeneo kadhaa lakini alisisitiza kuwa uamuzi wake ni wa busara na unatoa funzo kwamba siasa si uadui.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rugwe alisema inahitaji muda kumwelewa Lowassa akisema ziara yake Ikulu inahitaji kukaa naye na kungumza kabla ya kumshambulia au kufanya chochote.

“Unajua kipindi anajiuzulu uwaziri mkuu nafikiri alifanya vile kwa hasira baada ya kuona ile kamati iliyokuwa na uwezo wa kumhoji haikufanya hivyo na hili la kwenda Ikulu kila mmoja anataka kwenda kuonana na Rais, ila je, alikwendaje ndiyo hoja iliyopo,” alisema Rugwe.

USULI

Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.

Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967 kisha akaendelea Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971 na kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mirambo, Tabora mwaka 1972–1973.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).

Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.

Alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990. Amehudumu ubunge wa Monduli kuanzia mwaka 1995 hadi 2015.

Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.