In Summary
  • Neema Matimbe (15) mama wa mtoto anayedaiwa kuishi kabatini kwa miezi mitano ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Rufaa Mkoani Dodoma lakini tayari imeibuka changamoto nyingine ya wapi eneo salama la kuishi Neema na mwanaye.Dodoma. Hatima ya sehemu atakayoishi mama wa mtoto wa miezi mitano ambaye inadaiwa alikuwa akitunzwa kabatini tangu azaliwe, ipo mikononi mwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mama huyo, Neema Matimbe, (15), mfanyakazi wa ndani wa Anitha Kimako ambaye ni mwalimu, amelazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu ya mwanaye.

Hospitali hiyo inatafuta sehemu salama kwa ajili ya kuishi binti huyo ambaye amemtuhumu mwajiri wake kuwa alimjeruhi na alikuwa akimshinikiza amuhifadhi mtoto wake kabatini, madai ambayo jeshi la polisi limeyapinga.

Tayari Anitha ameshafikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kushambulia, na yupo nje kwa dhamana.

Ofisa ustawi wa jamii wa hospitali hiyo, Theresia Lawei aliiambia Mwananchi kuwa mpaka sasa Serikali haijapata mahali pa kumpeleka binti huyo kwa ajili ya usalama wake na mwanaye.

Lawei alisema mtoto huyo anaendelea vizuri, lakini changamoto iliyojitokeza ni mahali pa kwenda kuishi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini kwa kuwa bado wanahofia usalama wake.

“Anaendelea vizuri yeye na mzazi wake. Tatizo linakuja mahali pa kwenda kuishi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, maana tunahofia usalama wake. Si unajua mazingira aliyokuwa anaishi,” alisema Lawei.

Ofisa huyo alisema japo Neema anatokea Wilaya ya Bahi, hawawezi kumruhusu aende huko moja kwa moja kwa kuwa hakuna mtu wa kumlinda.

Alisema kwa sasa mama mzazi wa binti huyo hayupo Bahi.

Mkuu wa idara ya watoto katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Muzzna Ujudi pia alisema Neema na mwanaye wapo vizuri ila anashindwa kuwaruhusu kwa sababu hawana mahali pa kwenda.

Taarifa zinaeleza kuwa juzi kulifanyika mchakato wa kumtambua kijana anayetajwa kumpa mimba na baadaye kumkataa. Polisi iliwapeleka vijana wawili katika wodi aliyolazwa mtoto huyo na Neema alimtambua.

Dk Muzzna alisema baada ya binti huyo kumtambua mzazi mwenzake alichukuliwa polisi.

Alisema jukumu lao ni kuendelea kutoa huduma kwa mtoto.