In Summary

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametumia hafla ya mapokezi ya ndege aina ya Airbus A220-300 kueleza jinsi anavyotamani siku akikua kuwa kama Rais John Magufuli


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba viongozi wa dini kumuombea ili akikua awe kama Rais John Magufuli katika utendaji na hekima zake. 

Makonda ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 11, 2019 katika hafla ya kupokea ndege ya pili  aina ya Airbus A 220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam.

Amesema miongoni mwa sababu zinazomfanya atamani kuwa kama Rais Magufuli ni jinsi kiongozi mkuu huyo wa nchi anavyotekeleza kila analoahidi, asiyeyumbishwa katika kusimamia anayoyaamua na kumweka Mungu mbele kuliko mengine.

“Lakini kubwa kuliko unaipenda Tanzania kuliko hata familia yako na sijui kama unapata hata muda wa kukaa nao,” amesema.

Makonda amesema kutokana na udogo wa eneo la uwanja wa ndege baadhi ya watu wamelazimika kubaki nje.

“Nilisema waliowahi kutoa ahadi na kuzitekeleza waje kuhudhuria hafla hii wamekuja kwa wingi na waliobaki nje ya uwanja inabidi kuwasamehe na waliobaki nyumbani ni ishara kuwa hata ahadi majumbani mwao wanashindwa kuzitekeleza,” amesema Makonda.