In Summary

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa mfanyabiashara Dewji amepatikana.


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha taarifa zinazodai kuwa Mohammed Dewji ‘Mo’ amepatikana lakini nyumbani kwa mfanyabiashara huyo watu mbalimbali wamekuwa wakiwasili.

Mwananchi limefika nyumbani kwa Mo maeneo ya Oysterbay jijini Dar es  Salaam na kushuhudia ndugu, jamaa na marafiki wakiingia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.

Nje ya nyumba hiyo kuna ulinzi mkali wa kampuni binafsi, lakini magari ya ndugu na jamaa na marafiki yamekuwa yakifika mfululizo.

Baadhi ya ndugu hao wakigoma kurekodiwa wamesema ndani kwa Mo hakuna taarifa sahihi kama amepatikana na kilichopo ni bado ndugu yao hajulikani aliko. Baadhi ya ndugu wa kike wamekuwa wakiingia huku wakilia.

Haha hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo aliyewahi kuwa mbunge wa Singida Mjini (CCM).