In Summary

Makonda ametoa maaigizo hayo le wakati akisikiliza kero za abiria katika kituo cha mabasi Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ni marufuku kwa dereva yeyote wa mabasi yaendayo kasi kuacha abiria vituoni.

Mabasi hayo ni yale ya ‘Express’ ambayo husimama vituo maalumu pekee.

Baada ya kusikiliza kero za abiria katika kituo cha Kimara-Mwisho, Makonda amesema haoni sababu ya madereva kuacha kuchukua abiria vituoni kwa sababu ni Express.

"Nimeshaongea na viongozi, hakuna haja ya gari kupita kwenye kituo na kuacha abiria. Kuanzia sasa hivi wanaotoa huduma za usafiri hakuna abiria kuachwa njiani," amesema.

Makonda amesema usafiri huo ulianzishwa kwa lengo la kurahisisha shughuli kwa wananchi na si kuwachelewesha kama hali ilivyo hivi sasa.

"Rais hakuwekeza mwendokasi ili watu wagombanie, aliwekeza mwendokasi ili watu wawahi kazini wakiwa safi,"amesema.

Hali ya usafiri katika kituo hicho haikuwa shwari kutokana na abiria kugombania mabasi.