In Summary

Kongamano hilo litafanyika Juni 26 na 27 mjini Mbeya

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika kongamano la biashara na uwezekaji kati ya Tanzania na Malawi.

 

Kongamano hilo litakalofanyika Juni 26 na 27 litawakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kwa lengo la kubaini fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.

 

Akizungumza leo jijini hapa mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema lengo ni wafanyabiashara na wawekezaji hao kubaini fursa ikiwemo kuanzisha na kuendeleza miradi katika sekta za viwanda, usafirishaji, utalii, uvuvi, kilimo, madini, elimu, afya, benki, mawasiliano na Tehama.

 

"Watu 500 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hili ambao ni  wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za umma na sekta binafsi kutoka Tanzania na Malawi,"amesema Makalla.

 

"Ofisi ya mkuu wa mkuu wa mkoa tutashirikiana na Kituo cha Uwekezaj Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTade) na taasisi ya biashara na uwekazaji ya Malawi.”

 

Mkurugenzi wa Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye  amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kwa maelezo kuwa kongamano hilo litatoa fursa ya kuanzisha viwanda ndani ya nchi na nchi ya Malawi.