In Summary
  • Dk Tulia asema vyama vya siasa vingine vimeshaeleza kile vinachoona kinafaa

Wakati mjadala ukiendelea kuhusu mawaziri kujibu hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), viongozi hao wameendelea kutoa ufafanuzi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na wa Kilimo, Dk Charles Tizeba leo Jumatatu Aprili 16, 2018 wametoa ufafanuzi wa hoja kuhusu wizara zao mjini Dodoma.

Kabla ya Mpina na Dk Tizeba kutoa ufafanuzi; Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe alisema sheria ya ukaguzi wa hesabu haimzuii waziri kueleza kilichoainishwa katika ripoti ya CAG.

“Hakuna dhambi kutoa maelezo maana ukaguzi wake ni wa mwaka 2016/17. Hivi tangu wakati huo mpaka sasa ina maana wizara haijafanya chochote kuhusu kilichoelezwa,” amehoji Dk Mwakyembe.

Amesema wanamuunga mkono CAG na kupongeza ripoti yake ndiyo maana kila mwaka wanazidi kufanya vizuri.

“Hati chafu zilikuwa nyingi miaka ya nyuma lakini safari hii hati chafu zipo tatu tu na wote wenye hati chafu wameshughulikiwa,” amesema Dk Mwakyembe.

Amesema wana wajibu kama Serikali kuwapa wananchi taarifa kwa mambo yanayowahusu.

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kujadili taarifa ya ukaguzi ya CAG si dhambi, ila kwa mawaziri wanapaswa kutoa majibu katika kamati za Bunge na wanachokifanya sasa ni kutoa maoni binafsi.

Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 16, 2018 alipojibu mwongozo wa wabunge Stanslaus Mabula (Nyamagana) na Goodluck Mlinga (Ulanga) waliohoji kama ni sahihi mawaziri kujibu taarifa ya CAG kwa maelezo kuwa majibu yao yanawachanganya wananchi.

Katika ufafanuzi, Dk Tulia amesema kinachofanywa na mawaziri ni sahihi lakini hayo ni maoni yao binafsi, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria ya ukaguzi, wanapaswa kutoa majibu katika vikao vya kamati za Bunge.

“Sheria kama ambavyo haimkatazi CAG kuzungumza na vyombo vya habari kwa namna hiyohiyo haimkatazi mtu yeyote kuzungumzia taarifa ya CAG, haijasema CAG azungumze na vyombo vya habari na pia haijamkataza mtu yeyote kuzungumzia taarifa hii,” amesema Dk Tulia.

Amesema, “Ndiyo maana vyama vya siasa vingine vimeshaeleza kile vinachoona inafaa. Sheria hizi mkizipitia waheshimiwa wabunge majibu huwa hayatolewi kwa mdomo. Waziri anatoa mawazo yake.”

Amesema anayepeleka taarifa ya CAG bungeni ni waziri, kwamba CAG hana mahali pa kupeleka hiyo taarifa isipokuwa kupitia kwa waziri.

“Kwa hivyo waziri anavyotoa maelezo si kwamba amejibu hoja za CAG, hoja za CAG zinajibiwa kwenye kamati kwa mujibu wa sheria, anayejibu kwenye kamati ni ofisa masuhuli husika,” amesema.

“Msitake kuliweka jambo hili kuonyesha hakuna utawala wa sheria nchini. Sheria zipo na mzisome vizuri kuliko kutoa maelezo ya kuchanganya umma,” amesema Dk Tulia.

Amesema, “Sheria ipo wazi kwamba ikishaletwa taarifa ya CAG hapa bungeni mtu yeyote ana ruhusa kuizungumzia. Hiki kinachojibiwa na mawaziri ni maoni yao.”