In Summary

Ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo 

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi nchini kuzingatia utaratibu wa ajira kwa kuajiri wafanyakazi wasiozidi watano wa kigeni la sivyo hatua zitachukuliwa kwa watakaokiuka.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 17, 2018 bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha papo kwa hapo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Leah Komanya.

Katika swali lake Komanya ametaka kujua kama Serikali iko tayari kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wafanyakazi kwa kigeni kuajiriwa na kufanya kazi maeneo nyeti kama viwanja vya ndege, bandarini na mipakani kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.

Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa nafasi kwa taasisi kuajiri wafanyakazi wa kigeni watano na nafasi hizo ziwe ambazo Watanzania hawawezi kuzifanya.

“Tumeweka ukomo ni wageni watano tu kwa taasisi ndiyo waajiriwe  kuitumikia na jambo hili linasimamiwa na tutahakikisha linafanyiwa kazi,” amesema.

“Katika maeneno yaliyotajwa na Komanya ni kweli yanahitaji kufanywa na Watanzania kutokana na kuwa nyeti hivyo nasisitiza Watanzania wanapaswa kutumika katika maeneno hayo ili kulinda usalama wa nchi.”

Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu amemuuliza Majaliwa hatua ambazo Serikali imezichukua kudhibiti elimu, nidhamu na malezi kwa shule binafsi.

Akijibu swali hilo Majaliwa  amesema ni kweli Serikali imetoa fursa kwa wawekezaji binafsi kutoa elimu ya msingi, sekondari hadi vyuo vikuu lakini kabla ya kuruhusiwa kutoa elimu hutakiwa kuzingatia miundombinu, usalama na mazingira ya kitaaluma.

“Kama mwekezaji huyu amekubali kuwekeza katika sekta ya elimu kama ni shule ya msingi, sekondari au vyuo lazima afuate mitalaa ya Serikali na tunao utaratibu wa kufanya ukaguzi ili kuona elimu inayotolewa inafanana na elimu ya shule zingine kwani mwisho kuna kipimo cha mitihani inayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa,” amesema Majaliwa.

Kuhusu malezi, Majaliwa amesema ,”Malezi na nidhamu tunaliwekea msisitizo kwani ndiyo tunajenga malezi. Serikali itaendelea kusimamia shule hizi kupitia vyombo vyetu kuhakikisha elimu inafanana na sote tunashuhudia yote yanakwenda sambamba kutoka pande mbili na malengo yetu kuhakikisa inatolewa kwa vijana wote wa Tanzania.”