In Summary
  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alitoa agizo kwa mkuu wa wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha anafanya uchunguzi wa kubaini matumizi ya fedha zinavyotolewa na Serikali kununulia dawa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri afanye uchunguzi kuhusu matumizi ya Sh70 milioni zinazotolewa kila mwezi na Serikali kwa ajili ya kununulia dawa kwenye wilaya hiyo.

Alitoa agizo hilo jana Oktoba 10, 2018 wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule Msingi Mpwapwa, ambapo alipokea malalamiko ya wananchi juu ya ukosefu wa dawa ambapo walidai dawa pekee wanazopewa ni za kutuliza maumivu tu.

"Kilichokuwa kinasemwa na wabunge bungeni nilidhani sicho, nikasema nakuja niyasikie mwenyewe. Kweli wananchi hawaridhiki nimeona. Sasa mkuu wa wilaya shughulikia hili jambo ili kubaini fedha za dawa zinakwenda wapi,” amesema. 

Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali kutoa fedha hizo kila mwezi ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya popote walipo badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda makao makuu ya wilaya. 

"Kila mwezi Serikali inatoa zaidi ya Sh70 milioni kwa ajili ya kununulia dawa kwenye wilaya hii ya Mpwapwa,” amesema.

“Pia, kuna fedha za mfuko wa afya Sh60 milioni pamoja na fedha za matokeo mazuri ya afya Sh300 milioni kwa mwaka, shida ya dawa haitakiwi kuwepo hapa,” alisema Majaliwa

Waziri Mkuu alibainisha Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu kama huduma bora za afya na ndiyo sababu ya kutoa fedha hizo za dawa. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwawa, Paul Swea kuwahamishia vijijini baadhi ya watumishi waliopo kwenye idara ya kilimo.

Alitoa uamuzi huo baada ya kubaini idara hiyo ina watumishi saba ambao wote wapo ofisini badala ya kuwepo vijijini na kuwasaidia wananchi kwenye shughuli za kilimo.

 Alimtaka mkurugenzi huyo kuandika barua za uhamisho kwa watumishi hao kwenda vijijini kisha nakala za barua hizo akabidhiwe kabla hajaondoka wilayani Mpwapwa na kusisitiza watumishi hao wanapaswa kwenda kufanya kazi na wakulima kwa karibu na kuhakikisha wanawapa elimu ya kutosha itakayowawezesha kulima kwa kisasa.