In Summary

Rais John Magufuli amesema kuna wakati anafuatilia hotuba za katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na kushangazwa na jinsi alivyo muwazi

 


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema kuna wakati anafuatilia hotuba za katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na kushangazwa na jinsi alivyo muwazi.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 11, 2019 katika hafla ya mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus220-300 iliyowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Magufuli amesema Dk Bashiru amekuwa muwazi na kufanya kazi kwa lengo la kuondoa dhuluma na ufisadi uliokuwa umetawala Tanzania.

“Vitu hivi vilikuwa vinazidi kukomaa kila siku, nakupongeza  pamoja na wana CCM wote kwa sababu mmefanya mambo makubwa ya kuisaidia Tanzania,” amesema Magufuli.

Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuwapa pole watendaji wa ngazi mbalimbali kwa kazi wanazozifanya pamoja na changamoto wanazokutana nazo na kuwataka kutokata tamaa kuwatumikia wananchi.

“Niwaeleze Tanzania katika miaka inayokuja itakuwa kama ulaya hivyo ninawaomba Watanzania muamini na haya yaliyopatikana katika miaka mitatu ni mvua za rasharasha tu mvua halisi zinakuja,” amesema Magufuli.

Amesema katika utawala wa mwalimu Julius Nyerere, walianza kununua ndege iliyokuwa na uwezo wa kubeba watu 19 kutoka Canada, kwamba hivi sasa ndege hiyo haijulikani ilipo.

“Sijui ilipotelea wapi, sasa hatutakubali kuona hizi ndege zilizotumia kodi za Watanzania zipotee, tunataka ziongezeke na kuleta maendeleo yatakayojenga,” amesema.