In Summary

Baada ya kupigwa biti na Bodi inayoendesha Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’kuwa haitakubali kuona kocha wa muda Santiago Solari akiendelea kuiongoza timu hiyo baada ya mapumziko ya kalenda ya Fifa katika ya mwzi huu, timu ya Real Madrid, imeanza mazungumzo na kocha wa zamani wa Monaco, Leonardo Jardim mwenye miaka 44 ili achukue nafasi ya Julen Lopetegui

Madrid, Hispania. Imefichuka kuwa klabu ya Real Madrid, imeanza mazungumzo ya kimya kimya na kocha wa zamani wa Monaco, Leonardo Jardim mwenye miaka 44 kuchukua nafasi ya Julen Lopetegui.

Jardim aliyeiwezesha Monaco kutwaa ubingwa wa Ufaransa msimu wa 2016-17 na kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, alibwaga manyanga mwezi uliopita kutokana na matokeo mabaya.

Madrid iliyomtimua Lopetegui, aliyeiongoza katika mechi 14 pekee, alishinda sita kufunga sita na kutoka sare mbili akikaa Santiago Bernabeu, siku 139.

Kipigo ilichokipata Real cha mabao 5-1 kutoka kwa Barcelona wiki mbili zilizopita ndicho kilichohitimisha ajira yake.

Klabu hiyo iliamua kumpa kocha wa timu za vijana za klabu hiyo, Santiago Solari kusimamia kikosi cha kwanza hadi kocha mkuu atakapotangazwa.

Tayari Solari ameanza vema kibarua chake alishinda mechi ya Kombe la Ligi Copa del Rey kwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Daraja la tatu ya Melilla, kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa La Liga dhidi ya Valladolid.

Bodi ya La Liga imeieleza Real kutafuta kocha mkuu haraka kwani Solari hawezi akaruhusiwa kuendelea kuiongozi timu hiyo baada ya mapumziko ya katikati ya mwezi huu kupisha mechi za kimataifa.

Hilo ndilo limemfanya Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, kuharakisha kumsaka kocha, ambapo awali alidaiwa kuwawania makocha kadhaa.

Kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte, kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez na yule wa Tottenham, Mauricio Pochettino, ambaye ameshasema hayupo tayari kujiunga na miamba hiyo, ndio wanaotajwa zaidi.

Hata hivyo taarifa za Jardim raia wa Ureno kubwaga manyanga Monaco zinaonekana kuongezea idadi ya makocha wanaopewa nafasi ya kutua Santiago Bernabeu.

Mlinzi chipukizi wa Real Madrid raia wa Morocco, Achraf Hakimi 20, anayecheza kwa mkopo Borussia Dortmund ya Ujerumani alisema anatamani kuona Solari akipewa kazi hiyo jumla.

Chipukizi huyo aliyepitia timu za vijana za Real Madrid chini ya Solari, alisema kwa mtazamo wake kocha huyo anaweza kuipa mafanikio makubwa.

Wakati hayo yakiendeela kiungo nyota wa timu ya Vissel Kobe ya Japan, Andres Iniesta, amemtumia salamu za pole na kuahidi kumuunga mkono kocha Lopetegui.

Iniesta alikuwa kiungo tegemeo la kocha huyo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania na alistaafu soka la kimataifa baada ya fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika huko Russia.