In Summary

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro limewasimamisha kazi watumishi sita wa halmashauri hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao zinazotokana na ubadhilifu  wa fedha huku ukimtaka Mkurugenzi wa  halmashauri hiyo (DED) kuwa mkali kwa watumishi na kusimamia ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo

Morogoro. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro limewasimamisha kazi watumishi sita kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya manunuzi yanayotia shaka.

Aidha baraza hilo limemuomba mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe kumtuma mkaguzi kwenda kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo inayotiliwa shaka ukiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo pamoja na kituo cha afya Mkuyuni na Duthumi.

Akisoma uamuzi wa Baraza hilo kwenye kikao cha baraza la madiwani mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakifanya kazi na kutoa uamuzi wanayoyataka kwa manufaa yao hivyo kuipa hasara Halmashauri.

Pamoja na kuwasimamisha kazi watumishi hao lakini pia baraza hilo limempa onyo ofisa ugavi wa halmashauri hiyo hivyo kuwataka watumishi wengine kufuata sheria, kanuni, miongozo na taratibu za utumishi.

Aidha alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwa mkali na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini mapema hujuma na ubadhirifu unaoweza kutokea badala ya kuwaachia watendaji wa halmashauri peke yao.

“Mkurugenzi naomba uwe mkali kwa watendaji na watumishi wako, yapo maneno mengi yanazungumzwa kuhusu watumishi na watendaji wako na tunapokwambia jambo naomba ulifanyie kazi, mwisho wa siku tutaonana wabaya, mtatuona wakorofi, mchelea mwana kulia hulia yeye,” alisema Kingo.

Katika hatua nyingine Kingo alimtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuisimamia kwa karibu idara ya manunuzi na kuhakikisha mapato yanakusanywa na kufikishwa halmashauri kwani wapo watumishi na wasiokuwa watumishi wanaokusanya mapato na kula fedha hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kayombe Lyoba alisema anaungana na uamuzi wa baraza hilo wa kuwasimamisha kazi watumishi sita huku akisema kwa sasa wataendelea kuwa watuhumiwa mpaka hapo mkaguzi atakapotoa taarifa yake dhidi ya tuhuma zinazowakabili watumishi hao.

Alisema yeye kama mkurugenzi amekuwa akisimamia kwa karibu ukusanyaji na matumizi ya fedha za miradi hata hivyo tuhuma hizo zimemfanya aweze kuongeza kasi katika kusimamia miradi yote ya halmashauri.