In Summary
  • Hoja kuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ukonga, Mwita Waitara alihamia chama hicho tawala kwa sababu alinunuliwa imeuteka mkutano wa kampeni za chama hicho leo Ijumaa Septemba 14, 2018 katika uwanja wa Mzambarauni, Gongo la Mboto.

Dar es Salaam. Hoja kuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ukonga, Mwita Waitara alihamia chama hicho tawala kwa sababu alinunuliwa imeuteka mkutano wa kampeni za chama hicho leo Ijumaa Septemba 14, 2018  katika Uwanja wa Mzambarauni, Gongo la Mboto.

Baadhi ya wabunge waliopanda jukwaani kumnadi Waitara ambaye alikuwa mbunge wa Chadema katika jimbo hilo tangu 2015 hadi Julai, 2018 alipojiunga CCM,  wamesema wanawashangaa wapinzani kubeba madai hayo yasiyo na mashiko.

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe amesema wapo viongozi wakubwa ambao waliihama CCM lakini hawakusema kwamba wamenunuliwa.

Amewatolea mfano baadhi ya viongozi hao kuwa ni mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema; Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa ambao kwa sasa ni wanachama wa Chadema.

Amesema viongozi hao walipohama CCM haikuzungumzwa kuwa wamenunuliwa.

"Kununuliwa ni hoja dhaifu sana, CCM inaheshimu demokrasia ndio maana haikusema neno viongozi hao walipohama. Kwa nini watu wao wakihama waseme wamenunuliwa?” Amehoji Bashe.

Bashe amewataka wapinzani kutoa ushauri juu ya mfumo sahihi unaotakiwa kutumika ili sheria zibadilishwe, kwamba kwa sasa wanatekeleza matakwa ya sheria na Katiba ya nchi.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa amehoji ni nani aliwanunua Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutokana na ya baadhi yao kumuunga mkono baada ya Julius Mtatiro kugombea kwa tiketi ya CUF.

 

"Wananchi msidanganyike na maneno yao. Mpeni Waitara kura zenu ili akawaletee maendeleo, atashirikiana na viongozi wa CCM katika kufanikisha hilo," amesema Kaluwa.

Naye mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amesema anatambua kazi iliyofanywa na Waitara katika jimbo hilo hasa katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali.

"Mchagueni Waitara tukalisukume gurudumu la maendeleo, tutaendelea kushirikiana katika kutatua kero zenu, ninamfahamu Waitara ni mchapakazi sana," amesema Ndugulile.